DODOMA-Wenyeji Dodoma Jiji FC ya jijini Dodoma imejikuta katika wakati mgumu baada ya kushushiwa kichapo cha mabao 4-0 na Mabingwa wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara, Young Africans Sports Club (Yanga SC).
Kichapo hicho walikipata Desemba 25,2024 katika Dimba la Jamhuri jijini Dodoma, matokeo ambayo yameiweka Yanga nafasi ya pili katika msimamo wa Ligi Kuu ya NBC.
Yanga ambayo imejikusanyia alama 36 ipo nyuma kwa alama moja dhidi ya watani zao Simba Sports Club ambayo ina alama 37 kwa sasa baada ya mechi 14.
Mabao ya Yanga SC yalifungwa na Clement Mzize dakika ya 19 ya kipindi cha kwanza huku la pili likipachikwa na Aziz Ki dakika ya 29 kwa mkwaju wa penalti.
Kabla kipindi cha dakika 45 za kwanza hakijafikia tamati, Mzize alirudi tena nyavuni dakika ya 38 na kuwaandikia waajiri wake bao la tatu.
Prince Dube dakika ya 62 alifunga mahesabu kwa kuwaandikia Young Africans Sports Club bao la nne ambalo lilidumu hadi dakika ya mwisho ya mchezo huo.
Tags
Dodoma Jiji FC
Habari
Ligi Kuu Tanzania Bara
Ligi Kuu ya NBC
Michezo
Yanga SC
Young Africans SC