ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, dhana ya Utalii wa Maadili inaendelea kukua zaidi kufuatia ujio wa viongozi mbalimbali wa kiimani nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na Mwanazuoni Dkt. Zakir Naik wa Taasisi ya Putrajaya ya Malaysia na ujumbe wake waliofika Ikulu kuonana naye.
Ameeleza kuwa, Zanzibar imekuwa na fursa kubwa ya kuendeleza utalii na ajira kwa vijana kufuatia utekelezaji wa dhana hiyo ya utalii wa maadili iliokubalika na jamii.
Rais Dk.Mwinyi amemsisitiza Mwanazuoni huyo kuyatembelea maeneo zaidi ya Kihistoria yaliopo nchini na kuwa Balozi wa kuitangaza Zanzibar Kimataifa.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi amemshauri Dkt.Zakir kufikiria kuitembelea Zanzibar Kipindi cha Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa lengo la kufanya Mihadhara kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu.