ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi amezikaribisha nchi za Umoja wa Ulaya, hususan sekta binafsi kuja Zanzibar kubaini fursa za uwekezaji ziliopo kwani kuna maeneo mengi hayajafikiwa hasa kwa sekta ya Uchumi wa Buluu kupitia Utalii, Bandari, Mafuta na gesi pamoja na sekta ya usafirishaji wa majini.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo tarehe 7 Disemba 2024, Ikulu Zanzibar alipozungumza na Ujumbe kutoka Kamisheni ya Umoja wa Ulaya ukiongozwa na Bi. Rita Laraujinha Mkurugenzi Mwendeshaji wa masuala ya nje, Kanda ya Afrika waliomtembelea.
Aidha Rais Dkt.Mwinyi amesema Zanzibar inadhamiria kuwa na umeme wa uhakika kutokana na kutanuka kwa shughuli za uchumi, miradi mikubwa ya maendeleo, ongezeko la hoteli za kitalii na kasi ya uwekezaji inayokuwa kila siku.
Rais Dkt. Mwinyi ameeleza kwa muda mrefu Zanzibar imekua ikipokea megawatt 100 za umeme kutoka Tanzania Bara kupitia waya za chini ya bahari ambao kwa sasa hautoshelezi, hivyo kuna kila sababu ya kupata umeme mbadala na kufikiria kuwa na umeme wa jua, mawimbi au upepo, hivyo ameuomba Umoja wa Ulaya (EU)kuangalia uwezekano wa kuisadia Zanzibar kwenye eneo hilo.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi ameusisitiza Umoja wa Ulaya kuiungamkono Zanzibar katika azma yake ya kukuza Uchumi kupitia sekta za kimkakati ikiwemo Uchumi wa Buluu na Utalii ambazo ni Sekta za kipaumbele kwa Serikali anayoiongoza.
Amebainisha kuwa kwa sasa Zanzibar inafanya utalii wa kisasa unaoshajihisha utalii wa kumbi za mikutano, utalii michezo na wa afya ambapo awali ilijikita zaidi kuendesha utalii wa fukwe na maeneo ya urithi ambao umezoeleka kwa muda mrefu.
Naye, Bi. Rita Laraujinha ameipongeza Zanzibar kwa ushirikiano wanaoutoa kwenye Miradi inayosimamiwa na EU na kumuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuwa wataendelea kuiunga mkono Zanzibar wa kuleta maendeleo hasa kwa masuala ya afya, elimu na Uchumi wa Buluu.