NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,mwaka 2024 ulikuwa wenye neema na mafanikio kwa Tanzania.
Ameyasema hayo Desemba 31,2024 huko Ikulu ndogo ya Tunguu jijini Zanzibar wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2025 kwa Watanzania.
"Uchumi wa nchi yetu uliendelea kuimarika na kuwanufaisha wananchi. Kati ya Januari hadi Juni 2024 uchumi ulikua kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023."
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, pia Deni la Taifa nalo liliendelea kuwa himilivu. Vilevile,mfumuko wa bei umebaki ndani ya lengo la asilimia 3, hali iliyochangiwa na sera madhubuti za kifedha.
"Tulishuhudia ongezeko la uwekezaji kutoka ndani na nje ya nchi. Kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania kati ya Januari hadi Novemba 2024, tumesajili miradi ya uwekezaji 865 yenye thamani ya Dola za kimarekani bilioni 7.7 inayotarajia kuzalisha ajira 205,000."
Amesema,Mamlaka ya Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Mauzo ya Nje (EPZA) imetoa vibali vya kuwekezwa nchini viwanda vipya vikubwa 15 vyenye thamani ya Dola za Marekani milioni 235.
Ni viwanda vinavyotarajia kuzalisha ajira karibu 6,000 na kuuza nje bidhaa zenye thamani ya Dola za kimarekani milioni 94 kwa mwaka.
Kwa upande wa mapato, Rais Dkt.Samia amesema, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kukusanya Shilingi trilioni 21.276 kati ya mwezi Januari na Oktoba, 2024 sawa na asilimia 99.3 ya lengo.
"Hili ni ongezeko la asilimia 17.5 ikilinganishwa na makusanyo katika kipindi kama hicho mwaka 2023. Mwaka huu pia tumeendelea na jitihada za kujenga uchumi wa kidijitali kupitia matumizi ya TEHAMA.
"Katika kufanikisha hilo, tumeunda Wizara mahsusi ya TEHAMA na tayari tumezindua Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali."
Rais Dkt.Samia amesema,miongoni mwa mipango ya baadaye katika kutekeleza mkakati huo ni kuhakikisha kuwa kila Mtanzania anatambulika kwa kutumia Jamii Namba, itakayotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA).
"Kuimarika kwa uchumi kumetuwezesha kuendelea kufanya mabadiliko chanya katika mifumo yetu wa Elimu Msingi na Sekondari hadi vyuo vya ufundi.
"Tumeendelea kusogeza huduma bora za afya karibu zaidi na wananchi, kutandaza zaidi miundombinu ya umeme, na kusambaza umeme vijijini."
Aidha, amesema wametekeleza dhamira ya kumtua mama ndoo kichwani, kwa kusimamia utekelezaji wa miradi 1,300 ya maji nchi nzima.
Rais Dkt.Samia amesema,kukamilika kwa miradi hiyo kutatufikisha kutimiza lengo la asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini.
Katika sekta ya kilimo, amesema walifanikiwa kuhamasisha kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara, kuboresha mifumo ya masoko ya mazao mbalimbali, na kupata bei nzuri ya mazao kwa wakulima.
"Kwa mfano, kwa mwaka 2024 ufuta uliuzwa kwa shilingi 4,850 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 3,600 mwaka uliopita 2023.
"Kahawa aina ya Arabika iliuzwa kwa Shilingi 8,500 kwa kilo ikilinganishwa na Shilingi 6,500 mwaka uliopita na kwa kahawa aina ya Robusta iliuzwa kwa Shilingi 5,000 kwa kilo badala ya shilingi 3,500 mwaka 2023."
Amesema,Mbaazi iliuzwa kwa Shilingi 2,236 kwa kilo mwaka 2024 badala ya Shilingi 2,000 mwaka 2023, kakao imeuzwa kwa Shilingi 35,000 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Shilingi 29,500 mwaka uliopita 2023.
Vilevile, korosho iliuzwa kwa Shilingi 4,195 mwaka 2024 ikilinganishwa na Shilingi 2,190 mwaka 2023, huku uzalishaji wa korosho unatarajiwa kufikia tani 425,205 kwa msimu wa 2024/2025 unaoendelea ikilinganishwa na tani 310,787 zilizozalishwa msimu uliopita wa 2023/2024.
"Mwelekeo wa Serikali ni kuboresha Mfumo wa Stakabadhi za Ghala kupitia soko la Bidhaa Tanzania (TMX) kwa mazao ya kilimo."