Afrika waipa kongole Tanzania uzalishaji wa mazao ya chakula

KAMPALA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema viongozi wa nchi za Afrika wameonesha matumaini makubwa na mikakati iliyowekwa na Tanzania katika kuzalisha mazao ya chakula yenye ubora hasa mpunga na mahindi.
Mheshimiwa Majaliwa amewahakikishia Wakuu wa Nchi na Serikali Barani Afrika kuwa Tanzania itaendelea kuimarisha masuala ya utafiti na kushirikisha sekta binafsi, taasisi za umma zinazojishughulisha na kilimo ili kuhakikisha nchi inakuwa tegemeo katika uzalishaji wa chakula barani Afrika.

Ameyasema hayo leo Jumamosi, Januari 11, 2025 alipomwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano Maalum wa Wakuu wa Nchi na Serikali za Umoja wa Afrika wa kupitisha Programu ya Kuendeleza Kilimo Barani Afrika (CAADP 2026 - 2035) uliofanyika katika kituo cha Mikutano cha Speke Resort, Munyonyo, Kampala nchini Uganda.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali imefarijika kusikia baadhi ya viongozi wa nchi za Afrika akiwemo Mheshimiwa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni wakiisifia Tanzania kwa kuzalisha mazao ya chakula yenye ubora na hasa mpunga na mahindi. “Haya ni mafanikio makubwa katika sekta ya kilimo nchini.”

“Natamani watu washindane kwa ubora katika uzalishaji, mfano mchele wa kutoka Tanzania ni bora zaidi na gharama yake ipo chini, kuna wakati walitaka nizuie usije lakini nikawataka nao wajitahidi kushindana katika uzalishaji wa bidhaa zenye ubora.

”Kauli ya Mheshimiwa Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni aliyoitoa wakati akiwasilisha hotuba yake katika mkutano huo, inatoa fursa kwa mataifa mengine kununua mchele kutoka Tanzania.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Tanzania imeweka mkakati wa kuhakikisha inaendelea kuzalisha chakula cha kutosha kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza ziada nje. “Kwa sasa kilimo chetu si cha kujikimu bali ni cha kibiashara.”Awali, Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni ametumia fursa hiyo kuwasisitiza Wakuu wa Nchi na Serikali wa Afrika kuhakikisha wanaongeza thamani ya mazao kabla ya kuyauza ili kuongeza tija na kukuza ajira hususan kwa vijana.
Ametoa mfano wa zao la kahawa, ambapo nchini Uganda kilo moja ya kahawa ghafi inauzwa dola mbili za Marekani, ambapo kahawa hiyo hiyo ikichakatwa bei inaongezeka na kuuzwa dola 40 za Marekani.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news