Baba Donald Trump, hebu pokea salamu

NA LWAGA MWAMBANDE

SIKU chache baada ya Rais wa Awamu ya 47 wa Marekani, Donald Trump kutoa tangazo la kujiondoa katika mradi wa ufadhili wa fedha katika Programu ya Kupambana na Virusi vya Ukimwi katika mataifa yaliyo na mapato ya wastani na ya chini, Shirika la Afya Duniani (WHO) limeelezea hofu yake kutokana na uamuzi huo.
Rais wa Marekani, Mheshimiwa Donald Trump.

Kwa mujibu wa WHO, mradi huo hutoa huduma za kuokoa maisha kwa zaidi ya watu milioni 30 kote duniani.

WHO imebainisha kuwa, kujiondoa kwa taifa la Marekani katika ufadhili wake kunawaweka waathiriwa wa maradhi ya Ukimwi katika hatari ya kifo na kusambazwa kwa wingi kwa maradhi hayo.

"Kusimamisha ufadhili wa pesa katika Programu ya Maradhi ya Virusi vya Ukimwi kunawatia waathiriwa wa ugonjwa huu katika mauti na kurudisha chini kila juhudi zilizopigwa za kukabiliana na kudhibiti kusambaa kwa maradhi haya na ikiwa ufadhili huu hautaendelea basi tutakuwa tumerudi nyuma.

"Ni katika enzi za miaka ya zamani ambapo watu walifariki kwa wingi kwa kukosa kinga hiyo miaka ya 1980 na 1990 kote duniani likiwemo taifa la Marekani.

"Tunaomba Serikali ya Marekani kutathimini na kuangazia msaada wake katika mataifa yanayokua,"ilifafanua sehemu ya taarifa hiyo ya WHO.

Licha ya kumpongeza Rais Donald Trump kwa kuchukua maamuzi yenye kurejesha maadili mema katika jamii, mshairi wa kisasa Lwaga Mwambande amemuomba Rais Trump kufikiria upya kuhusu suala hilo ambalo linagusa afya za mamilioni ya watu duniani. Endelea;

1:Baba Donald Trump, hebu pokea salamu,
Hongera hii tripu, kwamba yena wahudumu,
Umeanza chapuchapu, mengi mengine muhimu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

2:Lile jambo la jinsia, zetu sisi wanadamu,
Wengi tumekusikia, na ndivyo tunafahamu,
Hivyo linatuingia, asante hiyo nidhamu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

3:Marekani mko juu, kiuchumi twafahamu,
Mwataka mbaki juu, hayo fanyeni kwa zamu,
Kwa misaada wakuu, dunia mnahudumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

4:Shirika letu la Afya, duniani lahudumu,
Wale wa shida za afya, tena gharama ni ngumu,
Wazidi kuwa na afya, misaada yahudumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

5:Dawa zinazofubaza, virusi kwetu muhimu,
Vinatufanya twaweza, afya zetu zikidumu,
Hizo ukizipoteza, wengi unatupa sumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

6:Si rahisi peke yetu, kupata dawa vigumu,
Kwanza ni uwezo wetu, dawa hizo za kudumu,
Hukumu ya kifo kwetu, kama sasa inatimu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

7:Ufadhili kusitisha, kuzifunga zako timu,
Kwamba ndiyo wasafisha, utawala utadumu,
Jua wengi watufisha, hatuwezi tukadumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

8:Hiki kifua kikuu, chatutesa wanadamu,
Dawa kifua kikuu, gharama zake ni ngumu,
Tukiwa wakuukuu, kujimudu ni vigumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

9:Na dawa za malaria, nazo iwe ni katumu,
Jinsi tulifurahia, gonjwa haliwezi dumu,
Sasa unatuziria, mbu watunyonye damu!
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

10:USAID ni muhimu, vema izidi hudumu,
Kazi yake twafahamu, afya zetu zinadumu,
Bila hivyo kujikimu, itakuwa hali ngumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

11:Trump wewe mzazi, dunia unahudumu,
Tafadhali kula pozi, misaada weze dumu,
Tunaohitaji dozi, za kila siku zidumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

12:Ni kama una kisasi, jinsi ulivyo mgumu,
Mengi chanya yako hasi, yazidisha hali ngumu,
Hebu ipunguze kasi, hekima kwako idumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

13:Ninaamini ujumbe, huu wetu ni muhimu,
Tafadhali tukuombe, mpini wako muhimu,
Makaburi usichimbe, watu wale wangedumu,
Lakini hili la afya, hebu upya fikiria.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news