ZANZIBAR-Balozi wa Vijana Zanzibar, Mohammed Kassim Mohammed (Prince Eddycool) amewataka vijana kuwa wabunifu na kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi ili kujiajiri na kujiongezea kipato.
Alitoa wito huo wakati alipotembelea miradi ya kilimo ya vijana wa Baraza la Vijana Shehiya ya Miwani Wilaya ya Kati, na kusisitiza kuwa Serikali inatoa msaada mkubwa kwa miradi ya vijana, hivyo ni muda wa wao kuchangamkia fursa hiyo.
Prince Eddycool aliongeza kuwa vijana wana vipaji vya aina mbalimbali na iwapo watafanya kazi kwa bidii na kuvitumia vipaji vyao vizuri, wataanzisha miradi yao na kuajiri wengine.
Alisisitiza kuwa Zanzibar ina ardhi nzuri kwa kilimo na kwamba ikiwa vijana watatumia fursa hiyo vizuri watapata mafanikio makubwa.
“Kijiji chetu ni kizuri na ardhi yake inakubali kilimo mukiweza kuzitumia fursa za kilimo vizuri mutaweza kufika mbali katika maisha yenu."
Aidha, alimpongeza Rais wa Zanzibara na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kutoa fursa za maendeleo kwa vijana na kusema kuwa Serikali inaunga mkono juhudi zao katika kujiajiri na kuajiri wengine.
Akitoa maelezo ya miradi hiyo Seif Hassan Seif Makamu Mwenyekiti Baraza la Vijana Shehia ya Miwani alisema jumla ya vijana 35 wamekusanyika kushirikiana kuendeleza kilimo cha bamia na muhogo ili kujikwamua kimaisha na kuwatoa kwenye utegemezi wa familia zao na Taifa kwa ujumla.
Mbali ya mafanikio wanayoyapata kupitia mradi huo lakini wanakabiliwa na changamoto mbalimbali kama vile ukosefu wa ardhi yao wenyewe na tatizo la maji, kwani wanategemea mito iliyo karibu ambayo hukauka hasa wakati wa kiangazi.
Alisema, changamoto hizo zitawakosesha shughuli za kufanya na kuwa miongoni mwa vijana wasiyojishughulisha endapo hazitatuliwa.
“Hadi sasa eneo tunalolitumia sio la kwetu na wakati wowote tunalazimika kuondoka kama mmiliki atalihitaji eneo lake kwa shughuli nyengine.”
Zainab Salum Ahmad, mmoja wa vijana wa baraza hilo, alisisitiza umuhimu wa wanawake kujitahidi kiuchumi na kuacha kutegemea familia zao au waume zao peke kwani kufanya hivyo kunashusha hadhi yao.
Alisisitiza kwamba kwa kujitahidi na kushirikiana, manufaa ya miradi hiyo yatapatikana kama ilivyokuwa kwa miradi mingine iliyopita ikiwemo kilimo cha mahindi.