Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yatoa elimu ya fedha kwa kundi lenye mahitaji maalumu Dodoma

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendesha mafunzo kwa wanachama wa kundi lenye watu wenye changamoto ya kusikia lijulikanalo kama UMIVITA mkoani Dodoma.
Akifungua mafunzo hayo leo hii tarehe 28/01/2025, Afisa Mwandamizi Mkuu wa Uhusiano wa Benki Kuu, Bw. Lwaga Mwambande, amewashukuru wanachama wa UMIVITA kwa kuona umuhimu wa kujifunza kuhusu majukumu ya Benki Kuu.

Amesema kila inapowezekana Benki Kuu hutoa elimu kwa wananchi, wakiwemo watu wenye mahitaji maalumu kuhusu majukumu yake na mchango wa taasisi hii katika maendeleo ya uchumi na kuwataka watumie nafasi waliyoipata kujifunza ili waweze elewa na iwasaidie katika maisha yao.

Baada ya kupata kwa muhtasari wasilisho kuhusu majukumu ya Benki Kuu, washiriki hao 60 pamoja na wasaidizi wao, walijifunza kuhusu alama za usalama katika noti zetu ili kujiepusha na fedha bandia, mafunzo yaliyoendeshwa na Afisa Mwandamizi wa Benki, Bi. Bertha Mrisho.

Naye, Meneja Msaidizi wa Uchumi Tawi la Benki Kuu Dodoma, Bi. Angela Abayo, aliwaasa wanachama hao wa UMIVITA kujiepusha na kukopa mikopo katika taasisi ambazo hazijasajiliwa na Benki Kuu ya Tanzania, kwani taasisi hizo huwa na riba kubwa na matokeo yake husababisha fedheha kwa wakopaji.

“Benki Kuu inawaasa wananchi wote wa Tanzania kujihadhari na taasisi ambazo hazina leseni ya Benki Kuu. Msipende kukimbilia kupata mikopo kwa masharti nafuu ambayo hayaeleweki, kwani mkumbuke kwamba hakuna fedha rahisi rahisi katika dunia ya sasa, hakikisha unakopa katika taasisi iliyosajiliwa na Benki Kuu pekee ili kujiepusha na mikopo inayoumiza na isiyolipika kwa urahisi,” alisema.

Mafunzo yameendeshwa kwa wanachama 60 wa UMIVITA Dodoma pamoja na wasaidizi wao, ambapo walijifunza kuhusu majukumu ya Benki Kuu, alama za usalama kwenye noti, masuala ya uchumi, na huduma ndogo za fedha.

Aidha, washiriki walipata fursa ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusiana na mada walizojifunza, jambo lililochangia uelewa mpana na majadiliano yenye tija.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news