DAR-Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Uthabiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha), Bi. Sauda Kassim Msemo, amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe kutoka Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania ukiongozwa na Balozi wake, Mhe. Charlotta Ozaki Macias, aliyeambatana na Makamu wa Rais Mwandamizi na Mkurugenzi Mtendaji wa Huduma za Kifedha wa kampuni ya Scania katika Kanda za Afrika, Mashariki ya Kati na Asia ya Kati, Bw. Lars Värnlund.

Akizungumza katika kikao hicho Naibu Gavana Msemo amesema Benki Kuu itaendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji katika sekta ya fedha ili kuhakikisha sekta hiyo inastawi kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi.
Naye, Mhe. Balozi Macias, ameishukuru Benki Kuu kwa kusimamia vizuri uchumi wa nchi na ameahidi kuendeleza ushirikiano uliopo kati ya Sweden na Tanzania kwa lengo la kuimarisha uchumi wa nchi zote mbili.