ZANZIBAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inashiriki katika Maonesho ya 11 ya Kimataifa ya Biashara ya Zanzibar, yanayofanyika katika viwanja vya Chamanangwa, Wilaya ya Wete, Mkoa wa Kaskazini Pemba, kuanzia tarehe 07 hadi 15 Januari, 2024.
Maonesho hayo, ambayo yalifunguliwa rasmi na Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mhe. Mudrick Ramadhani Soraga, ni sehemu ya maadhimisho ya Miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Benki Kuu inashiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa elimu na kukuza uelewa wa wananchi kuhusu majukumu yake.
Akimkaribisha Waziri Soraga kwenye banda la BoT, Mkurugenzi wa Tawi la Zanzibar, Bw. Ibrahim Malogoi, alisema Benki Kuu inatoa elimu kuhusu kazi zake, ikiwa ni pamoja na kusimamia na kutekeleza Sera ya Fedha, kusimamia sekta ya fedha, mifumo ya malipo ya taifa, na fursa za uwekezaji katika dhamana za serikali.