BoT yatoa rai kwa Ulaya na Afrika kushirikiana kutatua changamoto za kiuchumi

ZANZIBAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amehimiza ushirikiano kati ya Ulaya na Afrika katika kutatua changamoto za kiuchumi zinazojitokeza duniani.
Amesema hayo tarehe 29 Januari 2025 wakati akifungua Mkutano wa Tano wa Kamati ya Uangalizi wa Programu ya Ushirikiano kati ya Benki kuu za Umoja wa Ulaya na zile za Afrika (5th Program Steering Committee Meeting- The European System of Central Banks and African Central Banks).
Mkutano huo, unaozikutanisha Benki kuu kutoka mataifa 26 ya Afrika na Ulaya, unalenga kutatua changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza duniani.

Gavana Tutuba amesema mkutano huo ni fursa kwa washiriki kujengeana uwezo na kubadilishana uzoefu kuhusu namna mbalimbali za kutatua changamoto mbalimbali zinazoukumba uchumi wa dunia.
“Hapa Zanzibar tumepata washiriki kutoka mataifa 26 ambao kwa pamoja wanajadili masuala mbalimbali yanayochangia kutatua changamoto za kiuchumi duniani…Kwa hiyo mkutano huu ni fursa nzuri ya kubadilishana uzoefu ili kuimarisha uchumi wetu,” amesema.

Baadhi ya washiriki wa mkutano huo wanatoka nchi za Italy, Ufaransa, Uswisi, Ghana, Msumbiji na nchi nyingine ambazo zinafanya vizuri kwenye maeneo mbalimbali ya kiuchumi.
Aidha, ameongeza kuwa kikao hicho kitafanya tathmini ya mafanikio ya programu ya uangalizi katika kipindi cha mwaka mmoja kwa ajili kuboresha maandalizi ya programu nyingine yenye malengo kama hayo.

“Nimewaelekeza kuwa wasije wakaishia hapa, itakuwa vizuri taratibu kama hizi za kushirikiana kutatua changamoto za kiuchumi ziendelee kwa sababu dunia ipo kwa pamoja na changamoto zingine zipo nje ya uwezo wa mabenki,”amesema.

Ametoa mfano wa changamoto kama ya mabadiliko ya tabia nchi, kwamba haiwezi kutatuliwa bila kushirikiana kwa sababu ipo nje ya uwezo wa taasisi.
Mkutano huu wa kimataifa unafanyika katika ofisi ndogo za Makao Makuu ya BoT, Zanzibar na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Januari 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news