DAR-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imewataka wananchi wote kutumia Shilingi ya Tanzania wakati wanapofanya miamala yao nchini.
Pia, Benki Kuu ya Tanzania imesema ni kosa kununua, kuuza bidhaa na huduma hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni.
Aidha, kutumia fedha za kigeni kufanya miamala ya ndani ni kuhujumu uchumi wetu na kunufaisha sera ya fedha ya nchi za kigeni.
Gavana Tutuba ameyasema hayo leo Januari 8,2025 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wakuu wa benki na taasisi za fedha pamoja na waandishi wa habari.
Ni wakati akitangaza uamuzi wa Kamati ya Sera ya Fedha kwamba Riba ya Benki Kuu (CBR) kwa robo ya kwanza ya mwaka huu itabakia kuwa asilimia 6, kama ilivyokuwa katika robo mwaka iliyopita.
Gavana Tutuba amesema, Benki Kuu itaendelea kusimamia utekelezaji wa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Benki Kuu, 2006 kinachohimiza matumizi ya Shilingi katika kufanya miamala hapa nchini ili kupunguza mahitaji ya fedha za kigeni yasiyokuwa ya lazima.
Vilevile amesema, uamuzi huo ambao ulifikiwa katika kikao cha Kamati hiyo iliyokutana Januari 7,2025 jijini Dar es Salaam umefikiwa kutokana na tathmini ya mwenendo wa hali ya uchumi wa dunia na hapa nchini.
Kiwango hiki cha Riba ya Benki Kuu kinatumika wakati benki zinapofanya biashara ya fedha kati yao.
Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema hadi hivi sasa, Benki Kuu imeshanunua tani 2.5 za dhahabu ikiwa ni jitihada zake za kuongeza akiba yetu ya fedha za kigeni.Lengo ni kununua tani 6 hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu wa fedha 2024/25.