NA DIRAMAKINI
MKUU wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, Ester Mahawe amefariki dunia leo Januari 14, 2024 wakati akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini mkoani Kilimanjaro (KCMC).
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
"Nimepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha Mkuu wa Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe Mhe. Ester Mahawe.
"Kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ninatoa pole kwa familia, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, wafanyakazi na wananchi wote wa Wilaya ya Mbozi, ndugu, jamaa na mafariki kwa msiba huu. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi,” amesema.
Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kushirikiana na familia inaendelea kuratibu shughuli za mazishi na taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.