DCEA yakamata kilo milioni 2.33 za dawa za kulevya nchini

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema kuwa,kwa mwaka 2024 ilikamata zaidi ya kilogramu milioni 2.33 za dawa za kulevya.
"Hiki ni kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuwahi kukamatwa nchini na endapo kiasi hiki kingefanikiwa kusambazwa kingeleta athari kubwa na kuurudisha nyuma ustawi wa Taifa letu;

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo ameyasema hayo leo Januari 9,2025 wakati akitoa taarifa za dawa za kulevya nchini mbele ya waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa,mafanikio hayo yamechagizwa na juhudi kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kupambana na kudhibiti dawa za kulevya nchini kwa ustawi bora wa jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema,pamoja na ukamataji wa dawa hizo, DCEA ilijikita katika kutoa elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya na kuimarisha huduma za matibabu ya waraibu.

"Ni kwa kuongeza vituo vya huduma za tiba na utengamano na kuimarisha ushirikiano na wadau ndani na nje ya nchi."

Kamishna Jenerali Lyimo ameongeza kuwa,katika kipindi hicho bangi iliongoza kwa wingi katika ukamataji ikifuatiwa na methamphetamine, heroin na dawa tiba yenye asili ya kulevya aina ya Fentanyl.

"Aidha, kwa mara ya kwanza dawa mpya ya kulevya aina ya 3-4 Methylene-Dioxy- Pyrovalerone (MDVP) ilikamatwa nchini.

"Ufanisi huu ulitokana na operesheni zilizofanyika katika maeneo mbalimbali ndani ya nchi yetu ikiwemo eneo la Bahari ya Hindi ambapo dawa za kulevya zimekuwa zikiingizwa kwa kiasi kikubwa nchini kupitia majahazi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news