NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amesema,mwaka 2024 Diplomasia ya Tanzania ilizidi kuimarika na kuleta manufaa makubwa katika nyanja za kimataifa.
"Tumepata heshima ya kushiriki Mkutano wa G20, ambao pamoja na maamuzi mengine yaliyofanyika, mkutano huo pia uliazimia kuunga mkono jitihada za upatikanaji wa nishati safi.
"Vile vile, uliazimia kuimarisha uwekezaji kwenye kilimo ili kuondosha njaa na umaskini duniani,jitihada zinazoendana na malengo yetu Tanzania;
Ameyasema hayo Desemba 31,2024 huko Ikulu ndogo ya Tunguu jijini Zanzibar wakati akitoa salamu za mwaka mpya wa 2025 kwa Watanzania.
"Kwa mara nyingine tena, Tanzania iling’ara kwenye medani za kimataifa baada ya mgombea wetu Mheshimiwa Daktari Faustine Ndugulile kuwania na kushinda nafasi ya kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani, Kanda ya Afrika.
"Hata hivyo, kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu, Mheshimiwa Ndugulile alituacha kabla hata ya kuingia ofisini. Tunazidi kumuombea pumziko la amani."
Amesema,ziara walizozifanya katika nchi 16 duniani ziwezesha kujenga mahusiano ya kidiplomasia na kiuchumi.
"Ziara yangu nchini Jamhuri ya Korea, ilifanikisha kupatikana fedha zenye masharti nafuu kiasi cha Dola za kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya kutekeleza miradi katika sekta za maendeleo.
"Kupitia fedha hizo, pamoja na mambo mengine, tutajenga kituo cha kisasa cha mafunzo ya reli, chuo cha mafunzo ya anga na urubani, ujenzi wa kituo cha kusambaza umeme Nyakanazi, na kituo cha uchenjuaji wa madini na maabara za kisasa za vito."
Amesema,miradi mingine itakayoangaliwa ni mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Ujenzi wa Kongani ya Viwanda Bagamoyo, na Ununuzi wa Mabehewa ya Abiria na Mizigo kwa ajili ya Kipande cha Reli kutoka Mwanza hadi Isaka, Ujenzi wa Bandari ya Wete na Ujenzi wa Bandari ya Uvuvi Bagamoyo.
"Fedha hizo pia zitatumika kwenye Ujenzi wa Barabara Zanzibar, ujenzi wa Ukumbi wa Mikutano Zanzibar, na Ujenzi wa Studio ya Filamu ya Kisasa na Kituo cha burudani mbalimbali kwa ajili ya ajira za vijana.
"Ziara hiyo pia ilifanikisha kusainiwa kwa Mkataba wa masharti nafuu wenye kiasi cha Dola za Marekani milioni 163.6 kwa ajili ya kugharamia mradi wa Ujenzi wa Hospitali ya Binguni na Kituo cha Mafunzo ya Afya huko Zanzibar."
Rais Dkt.Samia amesema,ziara ya nchini China, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia ilifungua milango ya soko la bidhaa mbalimbali ikiwemo mihogo mikavu, soya, mabondo ya samaki, mazao ya baharini, asali, mashudu ya alizeti na pilipili.
"Ni matarajio yangu kuwa wakulima na sekta binafsi watachangamkia fursa hizi ili tuweze kunufaika na soko hilo.
"Wakati wa ziara hiyo, Tanzania, China na Zambia zilikubaliana kuifufua reli ya TAZARA ili kuboresha usafiri wa abiria na usafirishaji wa mizigo.
"Kwa upande wa ukanda wa SADC tulipata heshima ya kupokea Uenyekiti wa Asasi ya Siasa, Ulinzi na Usalama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, yenye jukumu la kusimamia masuala ya Ulinzi na Usalama katika Kanda hiyo, ambapo mbali na masuala mengine tumeweza kusimamia uangalizi wa chaguzi kwenye nchi za Botswana, Mauritius, Msumbiji na Namibia."