WASHINGTON-Rais mteule wa Marekani, Donald Trump pamoja na makamu wake, JD Vance wameapishwa rasmi kuliongoza taifa hilo lenye nguvu za kiuchumi na ushawishi mkubwa duniani.
Hafla ya uapisho imefanyika Januari 20,2025 huko Capitol jijini Washington DC majira ya saa 12 jioni kwa saa za Marekani.
Trump ambaye ni Rais mstaafu wa Awamu ya 45 wa Marekani, pia anakuwa Rais wa 47 kulitawala taifa la Marekani.
Ushindi wa Donald Trump mwenye umri wa miaka 78 akiwa ndiye mkuu wa nchi mzee zaidi wa Marekani kuwahi kuapishwa ulitokana na uchaguzi wa Novemba 5,2024 baada ya kumshinda Makamu wa Rais kutoka chama cha Democratic, Kamala Harris.
Donald Trump amekula kiapo mbele ya Jaji Mkuu John Roberts huku akiwa amegusa Biblia mbili zilizokuwa zimeshikwa na mke wake, Melania Trump.
Moja ya Biblia hizo iliwahi kutumika na Rais wa zamani wa nchi hiyo, hayati Abraham Lincoln wakati wa uapisho wake mwaka 1861 na Barack Obama mwaka 2009 na 2013.
Miongoni mwa vipaumbele vyake kwa sasa, Trump amesema ni kushughulikia changamoto za uhamiaji haramu huku akitarajia kutangaza dharura ya Kitaifa katika mpaka wa Kusini mwa taifa hilo.
Vilevile amesema, kazi ya kuwarejesha makwao mamilioni ya wahamiaji haramu nchini Marekani itaanza mara moja.
Pia,ameahidi kubadilisha jina la Ghuba ya Mexico kuwa Ghuba ya Marekani na Serikali itachukua udhibiti wa Mfereji wa Panama.
Trump pia amesema ataweka msukumo katika kushughulikia changamoto ya mfumuko wa bei na nishati ili kuwapa nafuu ya maisha wananchi.
Trump vilevile amesema ataweka sera rasmi ya serikali ya kutambua jinsia mbili pekee katika nchi hiyo ambayo siku za karibuni imekabiliwa na changamoto ya watu kubadili jinsia zao.
"Nitakomesha sera ya Serikali ya kujaribu kuweka makundi na jinsia nyingine katika jamii.Kuanzia leo, itakuwa sera rasmi ya Serikali ya Marekani kwamba kuna jinsia mbili tu, mwanaume na mwanamke."
Mbali na hayo,Rais aliyemaliza muda wake,Joe Biden ametumia dakika zake za mwisho madarakani kutoa msamaha kwa wanafamilia wake.
Amesema,familia yake imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi na vitisho visivyoisha, vikichochewa tu na nia ya kumuumiza.
"Kwa bahati mbaya, sina sababu ya kuamini kwamba mashambulizi haya yataisha.Familia yangu imekuwa ikikabiliwa na mashambulizi na vitisho visivyoisha.
“Ninatumia uwezo wangu chini ya Katiba kumsamehe James B. Biden,Sara Jones Biden, Valerie Biden Owens,John T.Owens na Francis W. Biden,msamaha huo haupaswi kuchukuliwa kimakosa kama kukiri kwamba walihusika katika kosa lolote,”amesema Joe Biden.