DAR-Kuelekea maziko ya bondia Hassan Mgaya yatakayofanyika leo katika maeneo ya Jeti Rumo jijini Dar es Salaam,uongozi wa Chama cha Mabondia umekuja na mitazamo tofauti kuhusu fedha za rambirambi.
Marehemu Mgaya atazikwa leo saa saba mchana jijini Dar es salaam, lakini Chama cha Mabondia kinachoratibu suala la mazishi na maziko hayo kimeonekana kukinzana kuhusu kuwekwa mchanganuo wa fedha za rambirambi ambazo huchangishwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kukabidhiwa kwa wafiwa.
Mwenyekiti wa Chama cha Mabondia nchini Tanzania, Japhet Kaseba amesema,kumekuwa na sintofahamu ya pesa zinazopelekwa kwa wafiwa bila wadau kujua imepatikana kiasi kilichopatikana kwenye michango yote na kile kilichowasilishwa kwa wahusika.
"Watu wameanzisha utaratibu wa kuchangisha pesa kwenye magroup ya WhatsApp wanachanganya na pesa ya Chama cha Mabondia ambayo ni laki mbili inayotolewa kwa familia ya bondia husika na pesa ya TPBRC na hupeleka kwa mfiwa au bondia aliyepata tatizo bila kusema kiasi gani kilichopatikana na mwisho wa siku watu kuanza kuhisi labda pesa zingine zimeliwa.
"Pesa inapokabidhiwa kwa wafiwa inatakiwa itamkwe palepale sisi Chama cha Mabondia tumetoa kiasi gani na michango ya magroup imepatikana kiasi gani na TPBRC imetoa kiasi gani kwa sababu hizi pesa ni mali ya mabondia na sio mali ya viongozi wa chama na itasaidia kuweka kumbukumbuku sawa ya mapato na matumizi ya chama chetu,"amesema Kaseba.
Kwa upande wake Mweka Hazina wa chama hiko, Cosmas Cheka amesema pesa ya mchango wa msiba si busara kuitangaza kwa ajili ya kulinda faragha ya tukio la msiba.
"Pesa ya mchango wa msiba haitangazwagi na haina ufahari kutangaza na wakitaka majukumu yangu wachukue mimi nimeshachoka,"amesema Cheka.
Pia Cheka ameweka wazi anavyotumia muda wake wa ziada na nguvu yake binafsi kwa ajili ya kufanikisha masuala hayo yanayowahusu mabondia.
"Nashindwa kupumzika kwa ajili ya kushugulikia masuala ya mabondia na muda mwingine natoa hadi pesa yangu mfukoni ili mambo yaende,"amesema Cheka.