DAR-Freeman Mbowe ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na mgombea wa nafasi hiyo uchaguzi ujao amesema, watu waliotaka kumpindua katika nafasi hiyo wana majibu zaidi kuliko yeye.
Mbowe ameyabainisha hayo kupitia mahojiano yaliyofanyika na kurushwa na UTV kupitia Kipindi cha Trumpet.
"Mimi watu kutaka kunipindua nimelisikia na ninalisikia, kwasababu sikuwa sehemu ya hao wanamapinduzi sijui ajenda yao walitaka kuibeba vipi.
"Kwahiyo nisingetamani kuingia kwenye mjadala huo, wao ukiwauliza wanaweza kuwa na majibu zaidi.
"Lakini dunia hii haina siri, vitu vya hila ni suala la muda tu na haki haijawahi kushindwa na uongo haujawahi kutamalaki.
"Huwezi kuwa kiongozi ambaye eti unataka kukiongoza chama kwa kuwashusha wenzio, kwa kuwakanyaga wenzako, kwa kuwatweza wenzako.
"Sisi ni binadamu, tuna mapungufu, yawezekana Mwenyekiti Mbowe ana mapungufu yake, Katibu Mkuu wangu ana mapungufu yake halikadhalika Wajumbe wa Kamati Kuu, kila binadamu ana mapungufu yake."
Wenje
Hayo yanajiri baada ya Mwenyekiti wa Kanda ya Victoria wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ezekiel Wenje kumjia juu Godbless Lema akidai ni miongoni mwa makada waliosuka mpango wa kumpindua Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe alipokuwa gerezani.
Wenje alidai kuna baadhi ya wanachama wa chama hicho, wakiongozwa na Mbunge wa zamani wa Arusha Mjini, Lema ambao walianzisha mpango uliopewa jina la Join the Chain.
Alisema, mpango huo ulikuwa na dhumuni la kukusanya fedha za kuwezesha kuitishwa kikao cha Baraza Kuu na Kamati Kuu ya chama hicho kuwashawishi wajumbe kufanya mapinduzi ya kumteua Tundu Lissu kuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa na Mchungaji Peter Msigwa awe Makamu Mwenyekiti wake.
Wenje ambaye pia ni mgombea wa nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa alidai hayo mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari.
"Mnakumbuka mimi, Lema na Lissu tulikimbia nchi, tukiwa huko mafichoni huku nyumbani mambo yakatokea mengi mpaka Mwenyekiti (Freeman Mbowe) akakamatwa akafungwa gerezani.
"Mwaka 2022, (Freeman Mbowe) akiwa gerezani, marafiki zangu hawa wakashauriana kwamba waanzishe kitu kinaitwa Join the Chain na mwenyekiti aliyeasisi hiyo movement ni rafiki yangu, Godbless Lema."
Aidha,Wenje alidai kuwa baada ya kushirikishwa mpango huo, aliamua kujiweka pembeni, akisisitiza uamuzi wake huo ukawa mwanzo wa matatizo na tofauti za kimtazamo kati yake na viongozi hao waliokuwa wakipanga njama.
"Niliposhirikishwa mambo kama haya, nilikataa uasi na hii ndiyo sababu kubwa ya kuanza kwa ugomvi mkubwa kati yangu na marafiki zangu, mimi nilikataa kuwa mwasi, nikajiondoa kwenye process yote."