DAR-Januari 21,2025 Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),kimefanya uchaguzi wa viongozi wake wa juu wa kitaifa kwa kuwachagua Tundu Lissu (Mwenyekiti), John Heche (Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara) na Said Mzee Said (Makamu Mwenyekiti Zanzibar).
Pia,John Mnyika ameteuliwa kwa mara nyingine kuwa Katibu Mkuu wa CHADEMA.Kuchaguliwa kwa viongozi hawa kunahitimisha mchakato wa uchaguzi ulioanzia katika vitongoji hadi ngazi ya taifa ambapo CHADEMA kimepata uongozi katika ngazi zote.
Uchaguzi huu umedhihirisha uhai na uimara wa CHADEMA.Sisi Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), tunawapongeza wanachama, viongozi na CHADEMA kwa ujumla kwa kufanya uchaguzi kwa uwazi, utulivu na weledi wa hali ya juu.
Tunavisihi vyama vingine vya upinzani nchini viige kilichofanywa na CHADEMA kuweka uhalali wa viongozi wa vyama hivi ambavyo vingine vina viongozi wa kudumu.
Tunapongeza ukomavu wa kisiasa aliouonyesha aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA, FreemanMbowe,aliyekiongoza chama hiki kwa miaka 21 kwa kukubali kushindwa na kukabidhi madaraka kwa amani.
Tunafahamu ulikuwapo msuguano mkubwa wakati wa kampeni na joto lilipanda hadi polisi wakaimarisha ulinzi kwa kiwango ambacho hakijapata kushuhudiwa.
Ila mwisho wa siku kila kitu kimekwenda kwa amani.Ni imani yetu kuwa Mwenyekiti Lissu atashirikiana na uongozi uliopita kuponya majeraha yaliyotokana na kampeni zilzopandisha joto ndani na nje ya chama.
TEF inaamini pia uongozi wa Mwenyekiti Lissu utaendelea kutetea uhuru wa vyombo vya habarinchini na kulinda tunu za taifa ambazo ni amani, umoja na mshikamano wa Watanzania.Mungu ibariki Tanzania.