Jaji Werema alikuwa mtu mwenye maono na alifanya maboresho katika mifumo ya kisheria nchini-Mheshimiwa Hamza Johari

DAR-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari ameungana na Viongozi mbalimbali wa Serikali kuaga mwili wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Mstaafu Mhe. Frederick Werema, ambapo amemkumbuka Jaji Werema kwa maboresho makubwa katika mifumo ya kisheria na haki nchini, huku akiimarisha Utawala Bora, Utawala wa Sheria na kuendeleza wataalamu wa sheria.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameyasema hayo katika Viwanja vya Karimjee, Jijini Dar es Salaam wakati wa Ibada ya kuaga mwili wa aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Mstaafu Mhe. Federick Werema aliyefariki Desemba 30, 2024, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa akipatiwa matibabu.

“Wakati alipokuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema alikuwa mtu mwenye maono na alifanya maboresho katika mifumo ya kisheria nchini pamoja na kuwaendeleza na kuwainua Wanasheria Chipukizi nchini,” amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa katika kipindi cha utumishi wake katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Jaji Werema alihakikisha kuwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inakuwa nguzo muhimu katika utawala wa sheria nchini.

“Alikuwa kiongozi aliesimamia masuala ya kisheria ya Serikali kwa kujitolea bila kubagua wala kuogopa na ilipobidi kuwa tayari kuwajibika, huku akpigania maslahi ya taifa letu kupitia ushauri wake wa kisheria huku akizingatia misingi ya sheria na haki za binadamu,”amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mgeni rasmi katika Ibada hiyo ya kuuaga mwili wa Jaji Werema, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, amewataka watanzania kuyaendeleza yale mazuri na mafaniko aliyopata marehemu Jaji Werema enzi za uhai wake.

Akiwasilisha salamu za pole kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, amewasihi watanzania kuendelea kumuombea marehemu na kuendelea kuyaenzi aliyoyatekeleza Jaji Werema katika tasinia ya sheria.

“Napenda niungane na Mhe. Rais kutoa pole kwa familia, Watoto ndugu na jamaa, tasnia hii ya sheria, chama cha Wanasheria na wote walioguswa na msiba huu,”amesema Mhe. Majaliwa.
Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa salamu za pole kwenye ibada hiyo amuelezea Jaji Werema kuwa alikuwa kiongozi shupavu, mchapakazi na mwenye msimamo katika kutekeleza utawala wa sheria nchini.

“Alikuwa kiongozi mwenye msimamo thabiti, ambaye hakusita kutoa ushauri muda wote kuhusu masuala ya sheria kwa maendeleo ya sekta ya sheria katika nchi yetu,”amesema Jaji Mkuu wa Tanzania.
Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Ally Possi ameeleza kuwa Jaji Werema atakumbukwa kama mtu aliyependa matokeo kwa kuonesha umahiri mkubwa katika kutekeleza majukumu yake kwenye kila wadhifa aliotumikia, kwa kuwa Marehemu Jaji Werema alikuwa tayari kupokea maoni ya watumishi bila kujali cheo katika kutatua changamoto mbalimbali za watumishi aliowasimamia katika nafasi zote alizofanyia kazi.

Mara baada ya Ibada hiyo mwili wa marehemu Jaji Werema,utasafirishwa tarehe 03 Januari 2024, kuelekea kijijini kwake Kongoto, Buswahili Mkoani Mara kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika tarehe 04 Januari 2024

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news