DODOMA-Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi amesema Tanzania na Japan zitaendelea kushirikiana kwenye Sekta ya Sanaa, Utamaduni na Michezo kwa kuanza kufundisha Lugha ya Kiswahili nchini Japani.
Kabudi amesema hayo wakati alipokutana na Balozi wa Japani nchini anayemaliza muda wake Mhe. Yasush Misawa alipotembelea ofisi za wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma.
Akielezea suala hilo, Waziri Kabudi amesema kuwa wizara itahakikisha lugha ya Kiswahili inaenea kwa kukifundisha na kuandaa vitabu vya lugha hiyo vilivyotafsiriwa kwa lugha ya Japan ambapo wizara kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na Kiswahili nchini zitaweka mikakati ya jinsi ambavyo watakikuza Kiswahili nchini Japani.
Katika hatua nyingine, Waziri kabudi ameomba Japani kuendelea kushirikiana na Tanzania katika biashara ya bidhaa za sanaa hasa michoro ya Tingatinga na Vinyago vya kimakonde na kuifanya dunia ijue vitu hivyo asili yake ni Tanzania
Naye balozi Yasushi Misawa ameishukuru Tanzania kwa kuwa washirika wazuri na Japani katika nyanja mbalimbali ambapo amekubali kuunga mkono picha za Tingatinga na Vinyago vya kimakonde kwa kuvisafirisha na kuuzwa nchini humo.
Vilevile Mhe. Balozi amesema upande wa michezo Japani itaendelea kuipa ushirikiano Tanzania kwa kuleta wakufunzi na vifaa hasa vya mchezo wa Judo.