DAR-Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza rasmi kuwa baada ya michezo ya Ligi Kuu ya NBC iliyofanyika Desemba 29, 2024, Ligi hiyo itasimama hadi Machi 1, 2025 itakaporejea kwa michezo ya mzunguko wa 17.
Kusimama kwa Ligi hiyo ni kutokana na kupisha michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi itakayofanyika kisiwani Pemba na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN), ambazo Tanzania ni moja ya nchi zitakazoandaa shindano hilo.
Bodi imejipanga kuhakikisha msimu wa 2024/2025 unafika tamati kwa wakati kwa mujibu wa kanuni za ligi, hivyo kutoathiri kipindi cha mapumziko na maandalizi ya msimu wa 2025/2026 kwa klabu zote.
Aidha, Bodi ya Ligi Kuu Tanzania inaamini klabu zake zitatumia kipindi hiki kufanya marekebisho na maboresho katika vikosi vyake ili kuendana na ushindani mkubwa uliopo kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu.
Bodi inaitakia kila la kheri timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars) katika michuano tajwa hapo juu huku pia ikiwatakia kheri ya mwaka mpya 2025 wadau wote wa mpira wa miguu zikiwemo klabu, mashabiki, wadhamini, vyama vya soka vya mikoa, vyama shiriki na watanzania wote kwa ujumla.