Lissu akabidhiwa ofisi

DAR-Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)Taifa,Tundu Lissu amekabidhiwa ofisi yake Januari 29,2025 na Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Lissu wakati wa kukabidhiwa ofisi hiyo, alikuwa na makamu mwenyekiti wake bara, John Heche na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Bolugwa.

Katika hafla hiyo Lissu alisema falsafa yake ya No Reform, No Election inaendelea na akawataka wanachama wote kuungana ili uchaguzi ujao uwe huru na haki.

Pia,alipoulizwa na wanahabari kwamba mbona siku zimekwisha alisema uamuzi wa kuunganisha nchi ya Tanganyika na Zanzibar ulifanywa na Bunge kwa siku moja tu na siku ya Jumamosi, hivyo hakuna sababu ya kushindikana kubadilisha mfumo wa uchaguzi kwa kusingizia muda.

Lissu alisema,hakuna haja ya kuingia kwenye uchaguzi huku wakijua kwamba watafanywa washindwe huku akiwakumbusha wanachama wao walivyofanyiwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika chaguzi zilizopita.
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Tundu Lissu amekabidhiwa Katiba ya TCD kama ishara ya kuanza rasmi majukumu yake mapya. Lissu anakuwa Mwenyekiti wa TCD baada ya kushinda uchaguzi katika chama chake, na hivyo anapokea kijiti kutoka kwa Mhe.Freeman Mbowe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa TCD kupitia CHADEMA, amekabidhiwa katiba hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Demokrasia Tanzania (TCD), Bi. Bernadetha Kafuko.

"Kwa sababu ya majukumu makubwa tuliyonayo mbele ya safari naomba mniruhusu nikaribishe wote ambao sio wanachama wetu wajiunge na CHADEMA tunahitaji nguvu kubwa tunahitaji jeshi kubwa zaidi mara dufu ya tulilonalo tunahitaji kila mtu alete karama, talanta zake kwenye hii kazi inayohitajika kufanyika kwa pamoja.

"Nikaribishe wote ambao kwa sababu mbalimbalo hawajawa bado wanachama wawe wanachama wetu.

"Tuna uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba na kuna No reform no Election(hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi).Hayo mambo mawili hayaendi pamoja hakuna mabadiliko hakuna uchaguzi sio hatutasusia uchaguzi tunaenda kujifungia tuijadili tuna chama haitakuwa uamuzi wa Tundu Lissu.

"Itakuwa ni uamuzi wa chama tutakaa viongozi tutakaa na Sekretarieti tutakaa na Kamati Kuu, tutatoka na msimamo ukitoka msimamo utakuwa ni msimamo wa chama.

"Ninachoweza kusema tu ni kwamba sasa inabidi tuzungumze lugha pekee anayoweza kuielewa Rais Samia Suluhu Hassan.”

Vilevile amesema, sababu iliyofanya wasemezane vibaya imepita, "sababu iliyotufanya tuvutane imepita na imepita kwa namna ambayo nchi hii nzima inaisifia.

"Nchi nzima hii inatusifia kwa hiyo kwa sababu tumefanya jambo ambalo kila mtu anatusifia bado tuna sababu ya kuvutana? Hapana."

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, John Heche amesema, “Nimememuona Mzee Wasira (Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara) amekuwa serikalini tangu akiwa na miaka 20 mimi sijazaliwa.

"Anataka atengeneze kama mabishano fulani na Mwenyekiti wetu wa taifa kwamba Wasira amshughulikie Lissu. Mzee Wasira Lissu atashughulika na Rais.

"Lissu anakuja kushughulika na Rais Samia hakuna nafasi ya Lissu kushughulika nawe. Wasira yule hawezi kuja na mawazo mapya kwa watu wamemaliza vyuo vikuu hawana ajira.

"Hakuna mtu atapata upendeleo kwa sababu alimuunga Lissu mkono na Heche tutachagua watu kutokana na uwezo, uwezo wako utakuweka kwenye nafasi tulihubiri mabadiliko na tutasimamia mabadiliko hakuna mtu ataonewa kwa sababu hakutuunga mkono kuweni na amani kabisa.

"Nataka niwaambieni wanachama wetu wanataka kutumia watu fulani hivi tupoteze muelekeo hiyo nafasi haipo.

"Tutawashughulikia sana, tutaacha kushughulika na CCM iwe tumekufa au tupo gerezani. Mtatunyamazisha tumekufa au tupo gerezani vinginevyo hakuna msalia mtume kwa hiyo msiwe na mashaka kwamba chama hakitaenda,"alidai Heche.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news