Madereva walevi wafungiwa leseni Dar

DAR-Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewafungia leseni za udereva madereva waliokamatwa kwa kipindi cha miezi sita baada ya kukutwa na kiwango kikubwa cha ulevi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,SACP Muliro Jumanne Muliro ameyasema hayo leo Januari 2,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini humo.

Ameeleza kuwa,hatua hiyo ni kwa mujibu wa kifungu 28 (3) (b) cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura 168 iliyofanyiwa marekebisho Mwaka 2002.

"Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeuanza mwaka 2025 vizuri na sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya zilikuwa za amani na utulivu.

"Hata hivyo usimamizi wa sheria na kanuni mbalimbali zikiwemo za usalama barabarani zilisimamiwa kikamilifu ili kudhibiti ajali za barabarani.

"Katika kipindi cha Sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya 2025, makosa hatarishi ambayo yangepelekea ajali yalidhibitiwa na kuchukiliwa hatua kwa wahusika, jumla ya madereva 179 walituhumiwa na kupimwa ulevi kati yao madereva 30 walikutwa na ulevi wa kiwango cha zaidi ya milligramu 80."

Amesema,kati yao madereva 22 walitokea Wilaya ya Kinondoni, madereva sita (6) Wilaya ya Ilala na madereva wawili (2) Wilaya ya Temeke.

SACP Muliro ameeleza kuwa, katika kipindi cha Novemba hadi Desemba 2024, jehi hilo lilifanikiwa kupata matokeo mahakamani ya watuhumiwa mbalimbali.

Ametaja miongoni mwao kuwa ni Sadick Foreni (30) mkazi wa Mbagala ambaye Mahakama ya Wilaya ya Temeke ilimuhukumu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.

Muliro amesema,Mahakama hiyo hiyo ya Temeke ilimuhukumu pia Joseph Ferdinand (35) mkazi wa Mbagala Kibonde Maji kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti.

Amesema kuwa, Ayub Hatibu (32) mkazi wa Tabata alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Kinyerezi miaka 30 jela kosa la kubaka huku Salmin Athuman (30) mkazi wa Kitunda akihukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Ameongeza kuwa,Henry Peter (36) mkazi wa Mbezi alihukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Ubungo miaka 30 jela kwa kosa la kubaka huku Ramadhan Amir (30) mkazi wa Kawe akihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.

Vilevile amebainisha kwamba, jumla ya watuhumiwa 250 walikamatwa kwa kuhusika na kuuza, kusafirisha na kutumia dawa za kulevya jijini Dar es Salaam.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news