DODOMA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Dodoma imeahirisha kesi ya mauaji ya mtoto Greyson Kanyenye (6) hadi Januari 27 mwaka huu, baada ya upande wa mashtaka kudai kuwa upelelezi wa shauri hilo bado unaendelea.
Kesi hiyo, yenye namba 35951, inawahusisha washtakiwa wawili, Kelvin Joshua (27) na Tumaini Msangi (28).
Akisoma shtaka hilo kwa mara ya pili, Wakili wa Serikali Patricia Mkina alieleza kuwa washtakiwa hao wanatuhumiwa kutenda kosa hilo Desemba 25, mwaka jana, katika eneo la Ilazo jijini Dodoma.
Mkina aliomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kusikiliza shauri hilo, kutokana na upelelezi ambao bado haujakamilika.
Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Daraja la Kwanza, Charles Eligi alisema kesi hiyo itatajwa tena Januari 27 mwaka huu, huku akisisitiza kuwa washtakiwa wataendelea kuwa mahabusu kwa sababu shtaka linalowakabili halina dhamana.
“Nimeahirisha kesi hii hadi Januari 27, mwaka huu, kutokana na sababu kwamba upelelezi bado unaendelea. Washtakiwa wote wawili wataendelea kushikiliwa mahabusu kwa kuwa shtaka hili halina kipengele cha dhamana.”
Greyson Kanyenye maarufu mtoto wa Chief Godlove, mfanyabiashara maarufu jijini Dodoma aliripotiwa kuuawa kwa kupigwa na kitu kizito kichwani usiku wa kuamkia Desemba 25, 2024 wakati mama yake akiwa matembezini.
Tags
Kurasa za Magazeti
Kurasa za Mbele na Nyuma za Magazeti
Magazeti
Magazeti ya Leo
Magazetini
Magazetini leo
Yaliyojiri Magazetini Leo