Makamu wa Pili wa Rais aweka jiwe la msingi ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kifundi Wilaya ya Micheweni

ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar,Mhe.Hemed Suleiman Abdulla amesema ujenzi wa miundombinu ya skuli za ghorofa zinazoendelea kujegwa ndani ya Mkoa wa Kaskazini Pemba zitasadia kuondoa changamoto ya msongamano wa wanafunzi madarasani na kuongeza kiwango cha ufaulu mkoani humo.
Ameyasema hayo wakati wa uwekaji wa Jiwe la Msingi katika Ujenzi wa Skuli ya Sekondari Kifundi Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini Pemba ikiwa ni muendelezo wa shamra shamra za kutimia miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Amesema, kuimarika kwa Sekta ya Elimu nchini kutawakomboa vijana wa kizanzibari kutoka katika umasikini kwa kuzalisha wataalamu wazalendo wa fani mbali mbali watakao lisaidia Taifa kupiga hatu zaidi kimaendeleo.

Mhe.Hemed amewataka waalimu kuwa na mioyo ya uzalendo katika kufundisha na kuwalea vijana katika malezi yenye maadili sambamba na kuwaahidi kuwa Serikali itaendelea kuyaangalia maslahi ya walimu kila nafasi itakaporuhusu ili kulinda heshima na hadhi ya waalimu nchini ikiwa ndio fikra na falsafa za waasisi wa mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Makamu wa Pili wa Rais amesema Azma ya Rais Dkt. Mwinyi ya kukifungua Kisiwa cha Pemba kiuchumi inaanza kuzaa matunda kwa wakezaji kutoka Mataifa mbali mbali kuonesha nia ya kuekeza Kisiwani humo hasa katika Mkoa wa Kaskazi Pemba jambo litakalisaidia kupatikana kwa ajira kwa vijana wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla.

Sambamba na hayo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameendelea kuwasisitiza wananchi wa Konde na Wazanzibar kwa ujumla kuendelea kudumisha Amani,upendo na mshikamano pamoja na kuyaenzi na kuyalinda Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ambayo ndio chachu ya maendeleo yaliyopo nchini.

Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema Bajeti ya Wizara ya elimu imeongezeka na kufikia Bilioni mia nane(800) kwa lengo la kuhakikisha watoto wa Kizanzibari wanasoma katika mazingira bora, skuli zenye hadhi na kukidhi mahitaji ya kusomea na kufundishia ikiwa ni dhamira njema ya waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Mhe. Lela amefahamisha kuwa siasa za chuki na hasama zimepitwa na wakati na hazina faida kwa Wazanzibari hivyo amewataka wananchi wa Kaskazini Pemba kuunga mkono na kuthamini jitihada za Rais Dkt Hussein Mwinyi za kuwaletea maendeleo.

Akisoma Taarifa ya Kitaalamu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Khamis Abdulla Said amesema Itakapomalizika skuli ya Sekondari Kifundi itakuwa na uwezo wa kuchukua wananfunzi 810 kwa mkondo mmoja kwa wastani wa wananfunzi 45 kwa kila darasa.

Khamis amesema Skuli hiyo ya ghorofa (G+1)inayojengwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Benki ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Afrika (BADEA) hadi kumalizika kwake itagharimu shilingi za Kitanzania Bilioni 9.47 itakayojumuisha madarasa, Ofisi za walimu, dakhalia mbili kwa wasichana na wavulana, mgahawa na vyoo zaidi ya 30 ambayo itasaidia kuondoa changamato ya wananfunzi kuingia skuli kwa mikondo miwili pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha ufaulu ndani ya mkoa huo.

Katibu Mkuu (WEMA) amesema samani na usafiri kwa ajili ya skuli ya Sekondari Kifundi vipo katika hatua ya mwisho ya mchakato wa manunuzi na vinatarajiwa kufungwa mara baada ya kukamilika kwa ujenzi wa skuli hio.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news