NA HAPPINESS SHAYO
WIZARA ya Maliasili na Utalii imetakiwa kushirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi katika kukuza soko la utalii nchini na kurahisisha utoaji wa huduma ya viza kwa watalii.
Hayo yamesemwa leo Januari 14,2025 na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Mhe. Timotheo Mnzava katika kikao kilichofanyika Bungeni jijini Dodoma.
“Wizara ya Mambo ya Ndani, Uhamiaji na Wizara ya Maliasili na Utalii mshirikiane kuikuza Sekta ya Utalii, tunahitaji mfanye zaidi kuisaidia sekta hii na kama kuna changamoto mkazitatue,” Mhe. Mnzava amesisitiza.
Mhe. Mnzava amezitaka Wizara hizo kuoanisha mifumo ya malipo kwa watalii na kuweka mikakati madhubuti ya kutambua masoko muhimu ya watalii na kuwavuta waje nchini sambamba na kurahisisha michakato ya kupata viza kwa watalii hao.


Kikao hicho kimehudhuriwa na Viongozi na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake pamoja na Viongozi kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Ndani ya Nchi na Uhamiaji.