Mbunge adaiwa kuwatuma Makatibu wake kusajili wapiga kura za maoni wapya Bunda

MARA-Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mbunge wa Jimbo la Bunda Vijijini kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Boniface Mwita Getere, amewaagiza Makatibu wa Chama hicho Kata na Vijiji kupita kwa wajumbe wa nyumba kumi wanaomuunga mkono ili waingize majina mapya manne kila Shina kwenye daftari la wanachama watakaopiga kura za maoni.
Chama cha Mapinduzi kimeelekeza kuwa mwaka huu kura za maoni zitapigwa kama ifuatavyo, Mabalozi na Wajumbe wanne wa Mashina, Kamati za Siasa Matawi, Kamati za Utekelezaji UWT Matawi, Kamati za Utekelezaji Wazazi Matawi, UVCCM Matawi, Mjumbe mmoja wa Mkutano wa Jimbo kutoka tawi, Wenyeviti wa Serikali za Mitaa na Vijiji, Kamati za Siasa Kata zote, Kamati za UWT Kata zote, Kamati ya Utekelezaji Wazazi Kata zote na UVCCM Kata zote.

Wengine wanaotajwa ni Wajumbe watano wa Mkutano Mkuu Jimbo na Kata, Kamati ya Siasa Wilaya, Kamati ya Utekelezaji UWT Wilaya, Kamati ya Utekelezaji Wazazi Wilaya, Kamati ya Utekelezaji UVCCM Wilaya, Sekretariet ya Wilaya, Madiwani na Wabunge viti Maalumu kama watakuwepo.

Baada ya kupata taarifa ya Chama haraka Mbunge amewatuma vijana wake, Katibu na Msaidizi wake kupita kwa Mabalozi au Wajumbe wa nyumba kumi ili kubadilisha majina ya wanachama wanne ili kuweka ambao wanaaminika kuwa wanamuunga mkono.

Hata hivyo, mpango huo umezusha taharuki kwa viongozi na wanachama wa Kata na Vijiji, baada ya kutekelezwa kwa kasi kubwa, ambapo wajumbe wa nyumba kumi waliofikiwa na Makatibu waliotumwa na Mbunge tayari wamejaza majina ya wanachama ambao inaelezwa kuwa watahusika kupiga kura za maoni za CCM mwaka huu.

Zoezi hilo ambalo linaendelea kwa usiri mkubwa limeanzia Kata ya Nyamuswa, ambapo Katibu wa Chama, Changwe Bita na Msaidizi wake Mugabo Musira wametumwa kuratibu zoezi hilo ambalo litaendelea kwa Kata saba za Jimbo la Bunda, lengo likiwa kuweka majina ya Wajumbe wanaowaamini kuwa watamchagua tena Mbunge huyo. Jimbo la Bunda lina Kata za Nyamuswa, Ketare, Hunyari, Mugeta, Nyaman'guta, Salama na Mihingo. Kila mjumbe wa nyumba kumi anatakiwa kutoa majina ya wanachama wanne ambao wanawaamini.

Mmoja wa Wajumbe wa nyumba kumi, ambaye anatoka Kitongoji cha Shuleni Kata ya Nyamuswa, baadhi ya majina ya wanachama walioingizwa kwenye daftari la wanachama yalikataliwa kwa madai kuwa majina yaliyopendekezwa si watu wa Mbunge, kitendo ambacho kimezusha taharuku.

Alipoulizwa kama ana taarifa ya kuwepo kwa zoezi hilo la kusajili majina ya wanachama waliopendekezwa na wajumbe wa nyumba kumi, Mwenyekiti wa CCM Kata ya Nyamuswa, Mohamed Kizuri, ameeleza kushangazwa na zoezi linalosimamiwa na Katibu wa CCM Kata ya Nyamuswa kwa agizo la Mbunge, akidai kuwa hajashirikishwa.

"Niko kwenye msiba, taarifa ya zoezi hilo hata mimi nimezisikia, baadhi ya wajumbe wasiokubaliana na kitendo hicho wamenipigia simu wakitaka kujuwa kama zoezi hilo lina baraka za chama, ukweli hata mimi kitendo cha kupita kwa wajumbe wa nyumba kumi wakitaka kubadilisha majina ya wajumbe kimenishangaza."

Mohmed amesema, baada ya kupata taarifa za malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama hususan ambao inaelezwa kuwa wanabaguliwa na kutolewa kwenye daftari la wanachama wa CCM, haraka aliwasiliana na Katibu ili kupata maelezo ya zoezi hilo, ambapo alijibiwa kuwa atajulishwa baada ya zoezi kukamilika. Amesema anashangazwa kwanini hakushirikishwa kwenye zoezi hilo wakati yeye ndiye Mwenyekiti wa Chama ngazi ya Kata.

Imethibitika kuwa Kata ya Nyamuswa ina vijiji vinne, lakini zoezi la kusajili majina ya wanachama ambao wajumbe wa nyumba kumi wanawaamini kuwa wanamuunga mkono Mbunge limefanyika katika vitongoji vya vijiji vya Nyamuswa, Makongoro A na Makongoro B. Lakini kwa upande wa kijiji cha Bukama, zoezi hilolinalofanywa kwa siri limekataliwa.

Taarifa za ndani zinaeleza kuwa Mbuge ameelekeza Kiongozi yeyote atakayehoji afukuzwe au kusimamishwa uongozi.

Ambapo katika Kata ya Nyamswa, tMwenyekiti wa UVCCM na Katibu wake wamevuliwa uongozi kwa maelekezo ya Mbunge baada ya kuhoji uhalali wa zoezi hilo.

Kitendo hicho si kwa Maslahi ya Chama cha Mapinduzi. Wanachama wamepaza sauti zao wakimuomba Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa kuingilia suala hilo, kwa sababu Wabunge hawana mamlaka ya kufukuza wanachama au kuwavua uongozi.

Mwezi Mei 2024 Mbunge huyo kutoka Bunda Vijijini, alizua gumzo katika Mitandao ya kijamii na wananchi baada ya kuiomba Serikali kuondoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu maarufu kama Boom, kwa sababu wanafunzi wanaopata Boom hawasomi, pia wana nidham mbaya na wanalewa.

Hoja hiyo ilizusha mjadala mzito kwa wabunge, wasomi wa kada mbali mabli na wananchi. Hata hivyo Chama cha Mapinduzi kilitoa msimamo kupinga kauli hiyo kupitia taarifa kwa Umma iliyotolewa na Amosi Makalla Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa Mei 9, 2024 kuwa huo ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.

Taarifa hiyo ilifafanua kuwa, “Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinapenda kuwajulisha wadau wote wa elimu na Umma wa Watanzania kuwa kitaendelea kuisimamia Serikali ili kuongeza utoaji wa mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu wenye sifa stahiki” Hata hivyo Serikali ya iliongeza pesa ya kujikimu, ‘boom’ kutoka Tsh 8,500/- hadi Tshs 10,000 kwa siku."

Chama cha Mapinduzi pia kiliuhakikishia Umma na Watanzania kuwa kitaendelea kuisimamia Serikali kutenga na kutoa pesa za kujikimu kwa wanufaika wengi zaidi wenye sifa stahiki.

Maoni ya kuondolewa kwa fedha za kujikimu hayatazingatiwa kwani hakuna haja ya kumpangia matumizi ya fedha mtu mzima. Taarifa hiyo iliongeza kuwa CCM itaendelea kupokea maoni ya namna bora ya kuboresha na kuimarisha mikopo ya wanafunzi.

Kwa siku za karibuni, Mbunge huyo amekuwa akikosolewa hadharani kuwa kwa kipindi cha miaka kumi alichosimama kama Mwakilishi wa Bunda hajaacha alama zaidi ya kutoa misaada ya majeneza ya kufanyia mazishi na kupeleka michele kwenye misiba, ambayo ni fedheha kwa wananchi wa Bunda.

Hivi karibuni mtu mmoja alishambuliwa kwa maneno ya wananchi alipoeleza msibani kuwa mama yake amezikwa vizuri kwa msaada wa jeneza lililotolewa na Mbunge,

Wananchi pia wanahoji sababu za kilichosimamisha kasi ya ujenzi wa barabara kuu ya Musoma, Nyamuswa Foti Ikoma. Mradi huo mkubwa baada ya kufika Salama umesimama na Mbunge hajawahi hata kuhoji kama wabunge wengine wanavyohoji sababu inapotokea miradi kama huo kusimama.

Ni dhahiri shahiri kuwa Mbunge wa Bunda ameshindwa kutimiza kile alichotumwa na wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news