DODOMA-Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb.), amesema wizara anayoiongoza imefanikiwa kuunganisha Mfumo wa Kidijitali wa Anwani za Makazi (NaPA) na mifumo mingine 13 ya kutolea huduma serikalini.
Waziri Silaa ameitaja baadhi ya mifumo iliyounganishwa na Mfumo wa NaPA ni mfumo wa TAUSI wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Block Management System wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, Nikonekt wa TANESCO, Posta Kiganjani wa Shirika la Posta Tanzania, Tfiber wa TTCL, Tanzanite Portal wa TCRA, PMS wa NEMC na LOIS wa EWURA.
Waziri Silaa alitoa taarifa hiyo Januari 20, 2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maazimio ya Bunge pamoja na utekelezaji wa Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2024/2025 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.
Aidha, Waziri Silaa amesema kwamba Wizara inaendelea na zoezi la uhakiki wa Anwani za Makazi na kukusanya taarifa za Anwani za Makazi za vituo vya utalii katika hifadhi tatu za Ngorongoro na 21 za TANAPA.
Waziri Silaa pia alieleza kuwa wizara imefanikiwa kujenga mifumo mitano (5) ya kitaifa ya kuwezesha wananchi kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Serikali. Mifumo hiyo ni Mfumo wa kisekta wa ubadilishanaji Taarifa ambayo ni mfumo wa Jamii X-Change na ZanXchange), na Mfumo wa Utambuzi Kidijitali (Jamii Namba).
Mifumo mingine ni Mfumo wa Utambuzi wa Wateja (e-KYC), Mfumo wa Malipo ya Kidijitali (Jamii Pay), na Mfumo wa Usajili na Uwezeshaji wa Wadau wa Ikolojia ya Tafiti na Bunifu za TEHAMA, ikiwa ni pamoja na Kampuni Changa (Safari Hunt).
Kwa upande wa mradi wa ujenzi wa minara 758 ya mawasiliano, Waziri Silaa alisema kuwa jumla ya minara 372 kati ya minara 758 iliyopangwa kujengwa imekamilika. Kati ya hiyo, minara 332 imewashwa na inatoa huduma katika maeneo mbalimbali nchini. Aidha, kwa upande wa minara 304 iliyopangwa kuongezewa nguvu yote imekamilika.