NA GODFREY NNKO
IMEELEZWA kuwa, watu zaidi ya milioni 7.2 wanaoishi mikoa nane kwenye halmashauri 30 nchini wako hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa wa Usubi.
Hayo yameelezwa hivi karibuni na Afisa Mpango, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP), Ruth Mchomvu katika mafunzo kwa wanahabari jijini Dar es Salaam.
Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP),lengo likiwa ni kushirikiana na vyombo vya habari katika kuelimisha jamii kuhusu magonjwa matano muhimu ambayo hayakuwa yanapewa kipaumbele nchini.
Magonjwa hayo ni matende na mabusha, trakoma, usubi, minyoo ya tumbo, na kichocho, ambayo bado ni changamoto kwa baadhi ya maeneo nchini licha ya juhudi za kukabiliana nayo kutoka kwa Serikali na wadau wa afya.
"Usubi ni ugonjwa unaoathiri ngozi na macho,unasababishwa na minyoo midogo sana iitwayo Onchocerca Volvulus. Minyoo hii huenezwa na nzi weusi wadogo wanaozaliana kandokando ya mito yenye maji yanayoenda kwa kasi."
Mchomvu amesema,mikoa hiyo ni Morogoro, Ruvuma, Mbeya, Songwe, Tanga, Iringa, Njombe, Iringa na Dodoma.
Amesema,Mkoa wa Morogoro halmashauri zilizoathirika na ugonjwa wa Usubi ni Morogoro Vijijini, Ulanga, Mlimba, Kilosa, Mvomero,Ifakara na Gairo.
Katika kuzuia hatari ya kupata ugonjwa huo, Mchomvu amesema ni muhimu kwa wananchi kumeza kingatiba za ugonjwa huo kila zinapotolewa kwenye jamii kwa kuwa dalili za ugonjwa huo huwa hazijtokezi mapema.
Vilevile kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma amesma ni Halmashauri ya Madaba, Songea Mjini, Songea Vijijini, Mbinga,Nyasa na Mbinga Mji.
"Mkoa wa Mbeya ni katika halmashauri za Tukuyu,Kyela na Busokelo, Mkoa wa Songwe ni Halmashauri ya Ileje.
"Kule Tanga ni halmashauri za Mkinga, Lushoto, Muheza, Bumbuli, Korogwe huku Iringa ikiwa ni halmashauri ya Mafinga.Mkoa wa Njombe ni katika halmashauri za Njombe Mji,Ludewa na Njombe na Mkoa wa Dodoma ni Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa,"amesisitiza Mchomvu.
Mbali na hayo, Mchomvu amesema kuwa, dalili za ugonjwa wa Usubi ni ngozi kuwasha,vinundu vinavyojitokeza kwenye ngozi,kukakamaa kwa ngozi mithili ya kenge.
Dalili nyingine,Mchomvu amesema ni ngozi kuwa na mabaka mabaka mithili ya mtu aliyeungua na moto au kama ngozi ya chui na kupata vipele ndani ya macho.
Amesema kuwa, dalili za ugonjwa wa Usubi huwa hazijtokezi mapema, hivyo ni muhimu kumeza kingatiba zake kila zinapotolewa kwenye jamii.
Mchomvu ameongeza kuwa,miongoni mwa madhara ya ugonjwa huo ni ngozi kuharibika, uoni hafifu na hatimaye ulemavu wa kutokuona.
"Pia, kushindwa kufanya kazi, hali inayosababisha umaskini katika kaya na jamii na kumfanya mtu kuwa tegemezi. Kwa hiyo, ugonjwa wa Usubi ni hatari na unatibika endapo ukikutana au kumuona mtu mwenye dalili za ugonjwa wa Usubi.
"Tafadhali mshauri aende kwenye kituo cha huduma za afya kwa ajili ya uchunguzi, matibabu na ushauri,"amesisitiza Mchomvu.
Siku ya Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele Duniani, yanayaadhimishwa Januari 30, 2025 yakiwa na kauli mbiu “Tuungane. Tuchukue hatua. Tutokomeze Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele.”