DODOMA-Katika kuhakikisha elimu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) inatolewa kwa viwango vya kisasa, Tume ya TEHAMA nchini imehakiki mitaala 21 katika vyuo mbalimbali nchini.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga akiwasilisha taarifa ya utekelezaji ya taasisi yake mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu jana bungeni jijini Dodoma.
Uhakiki huo, kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga, unaangalia kama mitaala hiyo imetatua ombwe lililokuwepo kwa kutokuwepo kwa wataalamu wa teknolojia ibukizi kwenye soko la ajira nchini.
Dkt. Mwasaga aliyasema hayo bungeni Dodoma jana wakati akiwasilisha Taarifa ya Utekeleza ya Tume ya TEHAMA mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu.Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mh. Jerry Silaa akifafanua jambo wakati wa kikao cha kupokea taarifa ya utekelezaji wa Tume ya TEHAMA bungeni jana mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyoketi chini ya uenyekiti wa Mhe. Moshi Kakoso.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kuduma ya Bunge ya Miundombinu, Mh. Moshi Kakoso (kulia) akifuatilia wasilisho la utekelezaji wa majukumu ya Tume ya TEHAMA jana bungeni jijini Dodoma. Wasilisho hilo lilifanywa na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA, Dkt. Nkundwe Mwasaga aliyeshuhudiwa na viongozi wakuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, wakiongozwa na Waziri wake, Mhe. Jerry Silaa.
Alisema uhakiki huo na juhudi nyingine zinazofanywa na Serikali kupitia Tume ya TEHAMA, zinalenga katika kutoa elimu ya uhakika kwa Watanzania, hususani vijana ambao ndio walaji wakubwa wa sekta hiyo inayokua kwa kasi duniani.
Sambamba na hilo, alisema uelewa wa vijana kuhusu umuhimu wa TEHAMA unaongezeka kwa kasi na kwa sasa Tume ya TEHAMA imesajili wataalamu wa TEHAMA 1,600 kwenye kanzi data ya taifa ya wataalamu.
“Hii inawezesha kuwajengea uwezo kwenye maeneo mbalimbali ya TEHAMA,” alisema Mwasaga na kuongeza kuwa, katika eneo hilo ya kuongeza ujuzi kwa wataalamu wa TEHAMA, tume ipo kwenye mazungumzo na shule na vyuo vya elimu ya uchumi Urusi ili kuweza kujengeana uwezo kwenye mafunzo ya maeneo mbalimbali ya ujuzi wa TEHAMA.
Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu, Mhe. Moshi Kakoso alionesha kuguswa na mkakati huo huku akihimiza kuhakikisha sekta ya TEHAMA inakuwa na ubora unaotakiwa.
“Dunia sasa hivi imeshabadilika. Tunahitaji wataalamu wengi. Mna Mawazo mazuri sana, lakini tunashauri ongezeko kasi katika kutekeleza dhamira ya Serikali ya kukuza Maendeleo ya Teknolojia ya sasa ni ya hali ya juu.
“Hawa vijana bado hatujawapa nafasi ya kutosha. Wakipewa ujuzi, wana mengi ya kufanya katika kuchangia mapinduzi ya kiteknolojia na kushiriki katika kuujenga uchumi wa kidigitali. Tuwaige Wachina, walipeleka vijana wengi sana nje ya nchi yao Kwenda kujifunza ujuzi kutoka kwa Marekani. Sasa hivi Wachina wako mbali mno na teknolojia inawalipa kwa sababu wamewekeza katika teknolojia,” alisema Mhe. Kakoso.
Tags
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Habari
Kamati ya Bunge
Mawasiliano na Teknolojia ya Habari
Tume ya TEHAMA