Balozi Dkt.Nchimbi mgombea mwenza urais, mfahamu kwa kina

DODOMA-Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameridhia kwa kauli moja kumpitisha Katibu Mkuu wa CCM Taifa Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi kuwa Mgombea mwenza (Makamu wa Rais) kwa Mgombea Urais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025.
Awali Rais wa Jamhuri ya Muungano wa  Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema,Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amemwandikia barua ya kuomba apumzike Umakamu wa Rais.

Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amesema, baada ya kutafakari ameridhia ombi hilo, lakini kwa sasa Dkt. Mpango ataendelea kuwa Makamu wa Rais hadi utakapofanyika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu 2025.

"Dkt. Philip Mpango ndiye Makamu wa Rais miezi ya karibuni hapa amekuja kuniona kuniomba apumzike, ana sababu kadhaa.

"Lakini sio za kazi, anasema yeye sasa ana miaka 68 na angependa kuishi zaidi, kwa hiyo naomba nipumzisheni, nikambishia bishia wiki iliyopita hapa akanikabidhi barua yangu hii (ya kujiuzulu) na barua sikumjibu, nilipoenda kwenye Kamati Kuu."

Balozi Dkt.Emmannuel Nchimbi ni nani?

Dkt. Emmanuel Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971 mkoani Mbeya,elimu yake ya Msingi aliianzia jijini Dar es Salaam katika Shule ya Msingi Oysterbay kati ya mwaka 1980 hadi 1986.

Baba yake mzazi, Mzee John Nchimbi kutoka wilayani Songea ni askari mstaafu wa Jeshi la Polisi na wakati anastaafu alikuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara. 

Mzee Nchimbi pia amewahi kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kwa vipindi viwili kupitia kundi la majeshi na baadaye katibu wa CCM wa mkoa, alikoma kushiriki masuala ya kisiasa mfumo wa vyama vingi ulipoanzishwa.

Dkt. Nchimbi alijiunga na elimu ya sekondari kwenye Shule ya Sekondari Uru kati ya mwaka 1987 – 1989 (kidato cha I – III) halafu akahamia Shule ya Sekondari Sangu na kukamilisha kidato cha nne mwaka 1989 – 1990.

Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari ya Forest Hill, Mbeya masomo ya kidato cha V na VI mwaka 1991 – 1993. Alijiunga katika Chuo cha IDM Mzumbe (Morogoro) na kuhitimu Stashahada ya Juu ya Utawala (mwaka 1994 – 1997).

Wakati anahitimu IDM, pia alichaguliwa kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na mwaka uliofuatia (1998), alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM).

Dkt. Nchimbi amewahi kuajiriwa na Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC) kati ya mwaka 1998 – 2003.

Alisoma, shahada ya uzamili ya usimamizi wa biashara Chuo Kikuu cha Mzumbe mwaka 2001 – 2003 akibobea kwenye maeneo ya (benki na fedha).

Dkt Nchimbi aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda (mwaka 2003 – 2005) na (mwaka 2008 – 2011) alisoma na kufanikiwa kuhitimu shahada ya uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Mzumbe.Dkt. Nchimbi amemuoa Jane na ni baba watoto watatu.

Mbio za ubunge

Dkt.Nchimbi alirudi nyumbani kwao (Songea Mjini) kuanza harakati za ubunge tangu alipokuwa anaongoza UVCCM. Ilipotimu mwaka 2005, aliingia kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi akakutana na Edson Mbogoro wa Chadema aliyekuwa mpinzani wake mkuu. 

Dkt. Nchimbi alisaidiwa na mtandao mkubwa wa CCM na kupata ushindi wa asilimia 67.6 dhidi ya asilimia 30.5 za Mbogoro.

Mara tu baada ya kuwa mbunge, Rais Kikwete alimteua kuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, hii ilikuwa Januari 2006, alidumu kwenye wizara hiyo hadi Oktoba 2006 alipohamishiwa kwenye Wizara ya Kazi, Ajira na Vijana – hapa pia alikuwa Naibu Waziri tangu Oktoba 2006 hadi Februari 2008 kisha Wizara ya Ulinzi na Kujenga Taifa ambako pia alikuwa Naibu Waziri hadi Novemba 2010.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Dkt.Nchimbi alijitosa tena Jimbo la Songea Mjini. Kampeni za 2010 zilimnyima usingizi pamoja na kuwa chama chake kilikuwa kimechukua asilimia zaidi ya 90 ya vijiji, vitongoji na mitaa mwaka 2009.

Kama kawaida, alipambana tena na Mbogoro wa Chadema na kumshinda kwa mara ya pili, japo safari hii Dkt. Nchimbi akipoteza takriban ushindi wa asilimia 10 ukilinganisha na mwaka 2005. Katika uchaguzi huo, alipata asilimia 59.9 dhidi ya 37.48 za Mbogoro.

Upandaji vyeo wa Nchimbi uliendelea, Rais Dkt.Jakaya Mrisho Kikwete alimpa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo akiwa Waziri kamili, alidumu hapo hadi Mei 2012 alipohamishiwa Wizara ya Mambo ya Ndani kabla ya kujiuzulu Desemba 2013.

Aidha, baadaye aliteuliwa kuwa Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Misri na Brazil kuanzia 2016 hadi 2023 ambapo baada ya kustaafu aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa CCM nafasi ambayo anahudumu hadi leo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news