NA GODFREY NNKO
KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyokutana Januari 7, 2025 imetangaza Riba ya Benki Kuu (CBR) kuwa asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka huu wa 2025 ili kutimiza malengo ya kiuchumi katika kipindi hicho.
Gavana wa BoT ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya MPC ameyasema hayo leo Januari 8,2025 katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam mbele ya wanahabari na wadau mbalimbali wa Sekta ya Fedha nchini.
Gavana Tutuba amesema,kiwango cha Riba ya Benki Kuu kilichotangaza kinaendana na malengo ya kuhakikisha kuwa mfumuko wa bei unabakia ndani ya lengo la asilimia 5.
Sambamba na kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia lengo la asilimia 5.7 robo ya kwanza ya mwaka 2025.
Gavana Tutuba amesema,uamuzi huo wa kamati wa kutokubadili Riba ya Benki Kuu unalenga kuhakikisha kiwango cha ukwasi kinaendelea kuwa cha kutosha katika uchumi, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia 5.
"Na kuwezesha kuongezeka kwa kasi ya ukuaji wa uchumi kufikia takribani asilimia 5.7 katika robo ya kwanza ya mwaka 2025.”
Riba ya Benki Kuu (CBR) ni kiwango cha riba ambacho BoT hutumia kufanya biashara na benki za biashara nchini na huwa kama muongozo kwa riba zote sokoni.
Matumizi ya riba hiyo yalianza baada ya kuanzishwa mfumo mpya wa sera ya fedha inayotumia Riba ya Benki Kuu (CBR) mwezi Januari,2024 ikiwa ni miongoni mwa njia zinazotumika na BoT kudhibiti mfumuko wa bei nchini.
Vilevile,mfumo wa kutumia riba unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa Sera ya Fedha nchini.
Wakati huo huo, Gavana Tutuba amesema,MPC imeridhishwa na mwenendo wa uchumi wa hapa nchini kutokana na utekelezaji madhubuti wa sera za fedha na bajeti na maboresho ya kukuza uchumi.
Amesema,kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani kumechangia kuendelea kuimarika kwa uchumi.
Gavana Tutuba amesema,kuimarika kwa uchumi pia kulithibitishwa katika tathmini iliyofanywa na Kampuni ya Fitch Ratings mwezi Disemba 2024, ambapo uchumi umendelea kubakia katika alama ya B+ yenye matarajio ya kuendelea kuimarika.
Pia, IMF imeonesha kuridhika na mwenendo wa uchumi katika tathmini ya programu za Extended Credit Facility (ECF) na Resilience and Sustainability Trust (RST).
Amesema,Benki Kuu itaendelea kuhakikisha uwepo wa ukwasi unaoendana na mahitaji ya uchumi ili kufikia malengo ya kuwa na mfumuko wa bei mdogo na kuchagiza ukuaji wa shughuli za uchumi.
"Katika kufikia malengo haya, Benki Kuu itaendelea kufuatilia mwenendo wa uchumi na kuchukua hatua stahiki pale itakapohitajika."
Gavana Tutuba amesema,kamati itakutana tena wiki ya kwanza ya mwezi Aprili kwa ajili ya kutathmini mwenendo wa uchumi na kuamua Riba ya Benki Kuu itakayotumika katika robo ya pili ya mwaka kuanzia Aprili hadi Juni, 2025.