Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power umefikia asilimia 99.55-Waziri Mkuu

NA GODFREY NNKO 

WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Kassim Majaliwa amesema, Serikali imeimarisha vyanzo vya nishati na miundombinu ya mafuta na gesi kati ya Novemba, 2020 na Desemba, 2024.
Amesema,katika kipindi hicho cha utekelezaji wa Ilani ya CCM, Mradi wa Julius Nyerere Hydro Power umefikia asilimia 99.55, na unatarajiwa kufikia MW 2,115 baada ya kukamilika.

Kwa sasa, umeme wa MW 1,410 unaozalishwa na mradi huo, umeingizwa katika gridi ya Taifa na umeanza kutumika nchini.

Ameyasema hayo Januari 19,2025 jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha Novemba 2020 hadi Desemba,2024.

Ni mbele ya wajumbe wa Mkutano Mkuu Maalum wa CCM ambao umeongozwa na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

"Njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 400 yenye urefu wa kilomita 160 kutoka JNHPP hadi Chalinze imekamilika."

Pia,amesema Serikali imeongeza uunganishaji wa umeme kwenye taasisi zinazotoa huduma kwa jamii zikiwemo za elimu, biashara, pampu za maji, vituo vya afya na nyumba za ibada kutoka taasisi 23,140 mwaka 2020 hadi taasisi 49,123 mwaka 2024.

Vilevile, Serikali imeunganisha umeme kwenye vijiji 12,278 kati ya vijiji 12,318 sawa na asilimia 99.67 na vitongoji 32,827 kati ya 64,359 sawa na asilimia 51.

"Miongoni mwa vijiji na vitongoji vilivyonufaika ni pamoja na vijiji vya Mkoa wa Kigoma, ambao tarehe 17 Oktoba, 2024 tulishuhudia Mheshimiwa Mwenyekiti Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ukiongoza kuzima jenerata la mafuta na kuwasha umeme baada ya mkoa huo kuunganishwa kwenye gridi ya Taifa."

Waziri Mkuu amesema, pia Serikali imeunganisha Gridi ya Taifa ya Tanzania na gridi za nchi jirani za Kenya kupitia mradi wa Backbone Transmission Power Investment Project wenye msongo wa kilovoti 400 na Burundi na Rwanda kupitia mradi wa Rusumo wa MW 80.

Mbali na hayo amesema,utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bomba la Kusafirisha Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) ambao kwa ujumla umefikia asilimia 52.50 unaendelea.

"Serikali pia imezindua na kuanza kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024 2034.

"Hivi sasa ndugu Mwenyekiti, dunia nzima inakutambua wewe Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi kuwa ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

"Mwezi Mei, 2024 ulizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao unatoa mwongozo wa kitaifa wa kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034."

Kupitia utekelezaji wa mpango huo, Waziri Mkuu amesema nyumba 1,551, viwanda 57, magari 5,000 na taasisi tisa zimeunganishwa na mfumo wa gesi asilia nchini.

Aidha, mitungi 87,100 ya gesi ya kupikia na majiko banifu 4,200 yameshasambazwa.

"Vilevile, Serikali imeendelea kujenga miundombinu ya kusambaza gesi asilia na kufunga mifumo ya kupikia katika taasisi zinazohudumia watu zaidi ya 300 kama vile shule za sekondari, kambi za jeshi na magereza.

"Aidha, mitungi 452,455 na majiko banifu 200,000 yenye ruzuku ya asilimia 25 hadi 50 yamesambazwa katika kaya zilizo katika maeneo ya vijijini,"amefafanua Waziri Mkuu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news