DODOMA-Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),CPA Amos Makalla amesema, Mkutano Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) unatarajia kufanyika Januari 18 hadi Januari 19,2025 jijini Dodoma.
Mkutano huo utakuwa na ajenda tatu ikiwemo kuziba nafasi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara ambayo awali ilikuwa inashikiliwa na Abdulrahman Kinana ambaye alijiuzulu Julai 29,2024.
Akiongea Januari 7,2025 katika Ofisi ya Makao Makuu ya CCM katika ukumbi wa White House jijini Dodoma, CPA Makalla amesema, ajenda hizo ni kujaza nafasi ya Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara.
Pia,kupokea kazi za chama kuanzia mwaka 2022 hadi 2025 pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji Ilani ya Uchaguzi ya CCM.
Aidha,kuhusu mchakato wa kumrithi Kinana, amesema mrithi wa nafasi hiyo anatarajiwa kupatikana baada ya Kamati Kuu kuwasilisha mapendekezo ya jina kwa Halmashauri Kuu kisha Halmashauri Kuu kuwasilisha jina hilo kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu kwa ajili ya kupigiwa kura rasmi.
Kinana ajiuzulu
Awali,Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan alikubali ombi la Makamu wake (Bara) Komredi Abdulrahman Kinana kujiuzulu.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alisema katika taarifa yake mwaka jana kuwa,uamuzi wa Rais ulifuatia barua ya Makamu Mwenyekiti iliyoomba kupumzika.
“Kwa muda mrefu Kinana aliomba kuachia ngazi,” rais alisema. “Nilimteua na kuahidi haitachukua muda mrefu … naamini hii ni ahadi ambayo ninapaswa kutimiza.”
Kinana alichukua wadhifa wa makamu mwenyekiti wa chama tawala mwaka 2022 baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa wakati huo Philip Mangula kujiuzulu.
Katika maelezo yake, Rais Samia alimshukuru mwanasiasa huyo kwa mchango wake mkubwa kwa chama.