NA GRACE SEMFUKO
MAELEZO
MSEMAJI Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Gerson Msigwa amesema Ofisi yake inakuja na Meza ya Msemaji Mkuu wa Serikali ili kuruhusu Waandishi wa Habari na Wananchi kupata taarifa kutoka kwa Viongozi wakuu wa Wizara na Taasisi kuhusiana na maendeleo yanayofanywa na Serikali.
Bw. Msigwa ameyasema hayo Januari 10, 2025 wakati akifunga mkutano wa Wahariri wa Vyombo vya Habari uliohusu mafanikio ya ukuzaji wa uwekezaji na maboresho ya mazingira ya biashara 2024 na mwelekeo wa 2025, ulioandaliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.
“Mhe Rais aliturudishia Wizara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali nikajiuliza nitoke vipi! kwa hiyo nakuja na meza ya Msemaji Mkuu wa Serikali ambayo tutakuwa tunawaita Waheshimiwa Mawaziri, watakaa watazungumza na Waandishi wa Habari, na nataka niende mbali zaidi nataka mpaka Wananchi waweze kuuliza maswali moja kwa moja kwa waheshimiwa mawaziri.
"Tutatengeneza utaratibu mzuri kwa msaada wa teknolojia ili tutakapoanza meza hiyo, tuweze kuvifikia vyombo vyote vya habari kwa watakaoweza kuja na wasioweza kuja, yaani mtu aweze kufikiwa na taarifa popote alipo,” amesema Bw. Msigwa.
Amesema Serikali ya awamu ya sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inafanya mambo makubwa ya maendeleo, hivyo viongozi wanatakiwa kuyasema kwa wananchi ambapo kupitia meza hiyo watapata fursa ya kuyajua mambo mengi na kwa kuanzia, januari hii itaanza mikutano ya taasisi katika kutimiza lengo la wananchi kupata taarifa.
“Taarifa za meza hii zitafika mpaka kwenye vyumba vya habari, kwenye televisheni, na kwenye simu yako ya mkononi, nawasubiri wanasayansi watafute namna ya kuweza kufika na kwenye masikio, tukiweza na huko basi mambo yetu yatakuwa yanakwenda vizuri sana, lakini kabla ya hapo, mwezi huu kabla haujaisha tutaanza mikutano ya taasisi, ni katika jitihada za kuhakikisha mnapata taarifa za kutosha,”amesema Bw.Msigwa.
Aidha, amempongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo kwa kuandaa mkutano huo wa wahariri na kueleza kuwa, hiyo ni sehemu ya mkakati wa ofisi ya Msemaji Mkuu wa Serikali katika kuuhabarisha Umma kuhusu maendeleo yanayofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
“Ndugu zangu tupo hapa na Wahariri na Waandishi wa Habari, nina furaha sana kuona kazi kama hizi zinafanyika kwa sababu sisi wizara yetu ndio inayosimamia sekta ya habari na tungependa kuona kazi za kihabari zinafanyika vizuri kwa hiyo nimefurahi sana na nachukua nafasi hii kumpongeza Mhe.Waziri na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), kwa kazi kubwa wanayoifanya na nawahakikishia kwamba tutaendelea kuifanya mikutano hii mingi zaidi,” amesema Bw. Msigwa.