Mtwale asisitiza ubunifu katika kuandaa na kutekeleza mipango ya kukuza uchumi na uzalishaji

NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI

NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale amewataka Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kuwa wabunifu katika kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi inayolenga kutatua changamoto za uchumi na uzalishaji katika mikoa na halmashauri wanazozisimamia.
Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji na Wataalam wa Wizara za Kisekta wakimsikiliza Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale (hayupo pichani), wakati akifungua kikao kazi cha viongozi hao kilicholenga kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26.

Bw. Mtwale wito huo leo katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kilicholenga kujadili utekelezaji wa Mipango ya Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 pamoja na kuandaa mipango ya Mwaka wa Fedha 2025/2026.

“Sehemu za uchumi na uzalishaji katika mikoa ndio zinabeba dira ya ukuaji wa uchumi na maendeleo endelevu katika nchi yetu hivyo ni muhimu mipango yenu ilenge vipaumbele vya Serikali kwa kuzingatia uendelezaji wa uchumi mahalia,” Bw. Mtwale amesisitiza.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale akizungumza na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji (hawapo pichani) katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI jijini Dodoma, wakati akifungua kikao kazi cha viongozi hao kilicholenga kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26.

Bw. Mtwale amehimiza kuwa, katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na maandalizi ya Mipango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 ni vema mipango na bajeti za mikoa na halmashauri zikazingatia mwongozo wa bajeti na vipaumbele vya nchi ili kuakisi utatuzi wa matatizo ya kiuchumi yanayowakabili wananchi na taifa kwa ujumla.

Sanjari na hilo, amewakumbusha Makatibu Tawala hao Wasaidizi wa Mikoa kuwa, wanajukumu muhimu katika maendeleo ya taifa hivyo waendelee kutekeleza majukumu yako kwa weledi na uzito unaostahili ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa majukumu yao hususani katika kutatua changamoto za uchumi na uzalishaji kwenye mikoa na halmashauri wanazozisimamia.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya Bw. Said Maditto akitoa neno la shukrani kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale, mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kufungua kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26.
Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Iringa Bw. Elias Luvanda akijitambulisha kwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26 ambacho kilichofunguliwa na Naibu Katibu Mkuu huyo katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Ukuzaji wa Viumbemaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bw. Nazael Madalla akiwasilisha mada ya masuala ya ukuzaji wa viumbemaji, wakati wa kikao kazi kilicholenga kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26.

Kwa upande wake, mwakilishi wa makatibu tawala hao wasaidizi Bw. Said Maditto ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Mbeya amesema kuwa kitendo cha kufanya kikao kazi na wakurugenzi wa wizara za kisekta ni fursa ya kujenga ushirikiano wa kiutendaji katika kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi nchini.

Aidha, Bw. Maditto amemuahidi Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale kuwa watatekeleza kwa vitendo maelekezo yote aliyoyatoa pamoja na kutekeleza maazimio wakakayotokanayo katika kikao kazi hicho kwa lengo la kuandaa mikakati na mipango endelevu itakayokuza uchumi wa taifa.
Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta akieleza lengo la kikao kazi cha Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji na Wataalam wa Wizara za Kisekta, kabla ya kumkaribisha Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale kufungua kikao kazi hicho katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI jijini Dodoma.

Naye, Mkurugenzi wa Tawala za Mikoa Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bi. Beatrice Kimoleta amesema TAMISEMI iliona ni muhimu kukutana na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji pamoja na wakurugenzi wa Wizara za Kisekta kwa ajili ya kupata maoni, maono na mtazamo wa namna bora ya kuandaa na kutekeleza mikakati na mipango ya kukuza uchumi nchini.

Pia, Bi. Kimoleta ameongeza kuwa kikao kazi hicho kitatoa fursa ya kupitia utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/2025 ili kuona nini kimetekelezwa mpaka hivi sasa na ni changamoto zipi zifanyiwe kazi ili zisikwamishe utekelezaji wa bajeti hiyo.
Washiriki wa kikao kazi cha kujadili utekelezaji wa mipango ya bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 pamoja na kuandaa mipango ya mwaka wa fedha 2025/26, wakiwa katika picha ya pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI Bw. Sospeter Mtwale, mara baada ya Naibu Katibu Mkuu huyo kufungua kikao kazi chao kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais_TAMISEMI jijini Dodoma.

Kikao kazi hicho cha siku mbili kimeudhuriwa na Makatibu Tawala Wasaidizi wa Mikoa wa Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji kutoka mikoa 26, Wakurugenzi na Wakurugenzi Wasaidizi kutoka Wizara za Kisekta pamoja na Wakurugenzi na Wataalam kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news