MARA-Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza Johari ameshiriki maziko ya aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji mstaafu Frederick Werema yaliyofanyika leo Januari 4,2025 katika Kijiji cha Kongoto wilayani Butiama mkoani Mara.
Akizungumza wakati wa utoaji wa salamu za pole, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, amesema kuwa Jaji Werema alijitolea kwa hali na mali katika kuhakikisha kwamba Serikali inatekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria na kwa uwazi.
Alipambana na changamoto nyingi zilizokuwa zikiikabili tasnia ya sheria na hakusita kuanzisha mabadiliko yaliyoleta matokeo chanya kwa wananchi na taifa kwa ujumla. Huu ni urithi mkubwa ambao utaendelea kuwa mfano na msingi wa kazi yetu sote tunaoendelea nayo leo.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amesisitiza kuienzi na kuiendeleza misingi na mifumo ya sheria aliyoianzisha Jaji Werema kwa ustawi wa sekta ya sheria na taifa kwa ujumla.
“Kazi yake ni nguzo ya msingi kwa maendeleo ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kwa maendeleo ya sekta ya sheria nchini kwa ujumla,"amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mhe. Johari amesema marehemu Jaji Werema, ameacha alama isiyofutika katika tasnia ya sheria na Utumishi wa Umma nchini, atakumbukwa kwa mchango wake mkubwa kwa taifa katika masuala mbalimbali ya kisheria na utendaji wa haki.