DAR-Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Hamis Mwinjuma, ameweka wazi mipango mbalimbali ambayo Serikali inatekeleza ili kusaidia ukuaji wa muziki wa Singeli na kuhakikisha unavuka mipaka ya Tanzania.
Katika kikao na wadau wa muziki huo, akiwemo Masoud Kandoro maarufu kama Meneja Kandoro na mtangazaji maarufu wa vipindi vya Singeli, Samadu Abdalah, kilichofanyika ofisi za wizara zilizopo uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Mhe. Mwinjuma ameeleza mikakati ya kuboresha muziki huo.
“Muziki huu asili yake ni Tanzania na Umekuwa ukitambulisha utamaduni wa Tanzania,"amesema Mhe. Mwinjuma.
Mhe. Mwinjuma amesisitiza umuhimu wa kuboresha viwango vya ubora wa muziki wa Singeli ambapo ameeleza kuwa tayari amepokea na kusikiliza nyimbo zaidi ya 20 ambazo zitaanza kufanyiwa kazi ili ziwe na ubora wa kimataifa na ziweze kusikika mahali popote Duniani.
Aidha, Mheshimiwa Mwinjuma ametangaza mpango wa kuandaa Singeli Festival kwa ushirikiano na mamlaka ya mkoa wa Dar es Salaam. Festival hii itafanyika kwa kufunga mitaa kwa siku mbili hadi tatu, ikilenga kusherehekea muziki wa Singeli na utamaduni wake. Lengo ni kuhakikisha muziki wa Singeli unapata sifa na hadhi inayostahili, kwani ni muziki unaoshika kasi zaidi mtaani kwa sasa.