DAR-Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma akiambatana na Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga (Chuma) ametembelea kambi ya watayarishaji wa Tamthilia ya Huba Kampuni ya BigOne Entertainment inayoongozwa na Mtayarishaji Aziz Mohamed ili kuona hatua za utayarishaji wa tamthilia hiyo.
Mhe. Mwinjuma amefanya ziara hiyo mwishoni mwa wiki katika kambi hiyo iliyopo maeneo ya Victoria jijini Dar es salaam.
Mhe. Mwinjuma aliwapongeza watayarishaji hao kufuatia kazi nzuri wanayoifanya kwa zaidi ya miaka 9 tangu tamthiliya ya “Huba" ilivyoanza kurushwa katika Chaneli ya Maisha Magic Bongo kupitia Kisimbuzi cha DSTV.
Pamoja na hayo, Mhe. Naibu Waziri aliwasihi Wasanii wote nchini kufuata taratibu za kisheria kabla ya kuanza kutayarisha kazi ikiwemo kuchukua vibali vya utayarishaji kutoka Bodi ya Filamu ili kurahisisha upatikanaji wa maeneo ya uhalisia ya upigaji picha kulingana na uhitaji wa hadithi husika ili kuongeza thamani ya kazi zao.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri amewapongeza watayarishaji wa Tamthilia hiyo kwa kufungua milango ya kufanya kazi nje ya mipaka ya Tanzania ambapo hadi sasa wameshafanya kazi ya utayarishaji wa Tamthilia za “Aziza”, “Sultana” pamoja na “Kasri” zimetayarishwa nchini Kenya.
Kwa upande wake Kaimu Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dkt. Gervas Kasiga (Chuma), aliwapongeza watayarishaji hao na kuwasisitiza kuendelea kufanya kazi kwa weledi na ubunifu ili kukuza vipaji vyao pamoja na kuzidi kuipa hadhi ya kisanaa na kipato Sekta ya Filamu nchini Tanzania.
Kwa upande wa Mkurugenzi wa BigOne Entertainment-Aziz Mohamed alimshukuru Naibu Waziri Mhe. Hamis Mwinjuma kufuatia ziara hiyo na kuahidi kuendelea kufanya kazi zenye ubora zitakazoongeza chachu ya ukuaji wa Sekta ya Filamu na Michezo ya Kuigiza nchini Tanzania.