NECTA yatangaza Matokeo Darasa la Nne na Kidato cha Pili mwaka 2024

DAR-Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limesema,wasichana wameongoza kufanya vizuri katika mitihani wa Kidato cha Pili na wa Darasa la nne, kwa mwaka 2024.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dkt. Said Mohamed amesema, katika matokeo ya mtihani wa upimaji wa Kidato cha Pili jumla ya wanafunzi 680,574 kati ya wanafunzi 796,825 waliofanya mtihani huo wamefaulu, sawa na asilimia 85.41.

Amesema, wanafunzi hao wamefaulu kuendelea na kidato cha tatu kwa kupata madaraja ya I, II, III na IV, ambapo matokeo haya yanaonyesha kuwa, wasichana waliofaulu ni 367,457, ikiwa ni asilimia 54, huku wavulana wakiwa 313,117, sawa na asilimia 46.

Akielezea matokeo ya Mtihani kwa Darasa la Nne, Dkt. Mohamed amesema, jumla ya wanafunzi 1,320,227 kati ya wanafunzi 1,530,911 waliofanya mtihani wa Darasa la Nne, sawa na asilimia 86.24 wamefaulu kwa kupata madaraja A, B, C na D ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.9.

Dkt. Mohamed ameongeza kuwa, kati ya waliofaulu, wasichana ni 699,901 sawa na asilimia 53, na wavulana ni 620,326 sawa na asilimia 47.

Takwimu zinaonesha kuwa jumla ya shule 197 kati ya shule 20,036 za Msingi zimepata wastani wa Daraja E katika mtihani wa Darasa la Nne, ikiwa ndilo daraja la chini zaidi lenye alama kati ya 0 na 60.

Amesema, idadi ya shule zilizofanya vibaya zimepungua kwani mwaka 2023 zilikuwa 325.

“Wanafunzi wa kujitegemea waliofaulu upimaji na kupata sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne ni 4,205 sawa na asilimia 55.94, huu ni mwaka wa kwanza kwa Wanafunzi wa kujitegemea kutahiniwa upimaji huu.”

Mitihani ya Taifa ya kuwapima uwezo wanafunzi wa Kidato cha Pili na Darasa la Nne, ulifanyika mwezi Oktoba na Novemba, 2024 Tanzania nzima.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news