DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emanuel Tutuba amesema kuwa Noti Mpya za Tanzania zenye Saini ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (kushoto), akipokea Noti Mpya kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, elfu Mbili na shilingi elfu moja, kutoka kwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, Noti ambazo zitaanza kutumika sambamba na Noti zilizopo hivi sasa, kuanzia tarehe Mosi Februari, 2025.
Gavana Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Mhe. Dkt. Nchemba, Noti kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, Elfu Mbili na Shilingi Elfu moja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
“Mheshimiwa Waziri, ninayofuraha kukujulisha kuwa zoezi letu la uchapaji upya wa Noti kwa marejeo ya toleo la mwaka 2010, limekamilika na tayari tumewajulisha wananchi kupitia taarifa niliyoitoa kupitia Gazeti la Serikali” alisema Bw. Tutuba.
Gavana Tutuba alifafanua kuwa Noti hizo zitatumika sambamba na Noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango imebadilishwa na kuwekwa Saini yako Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na Saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania aliyestaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa Saini ya Gavana wa Benki Kuu wa sasa, Bw. Emmanuel Tutuba,” aliongeza Bw. Tutuba.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa Noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu,"amesema Dkt. Nchemba.
Mhe. Dkt. Nchemba aliridhia Noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa tarehe moja Februari mwaka huu.
Tags
Benki Kuu ya Tanzania
Dr Mwigulu Lameck Nchemba
Governor Emmanuel Tutuba
Habari
Noti Mpya
Wizara ya Fedha Tanzania