Noti zenye saini mpya zitatumika sambamba na zilizopo kwenye mzunguko-Gavana Tutuba

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, amesema kuwa Noti Mpya za Tanzania zenye saini za Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaendelea kutumika sambamba na zile zilizopo kwenye mzunguko kuanzia tarehe 1 Februari 2025.
Gavana amesema hayo wakati akimkabidhi Waziri wa Nchi , Ofisi ya Rais Zanzibar (Fedha na Mipango), Mhe. Dkt. Saada Mkuya (Mb), noti za kifani za shilingi 10000, 5000, 2000 na Shilingi elfu moja.

“Mheshimiwa Waziri, tunatarajia noti hizi zitaingia kwenye mzunguko tarehe 1 Februari mwaka huu na katika kuzisambaza tunawafahamisha wananchi kwamba noti hizi zitaendelea kutumika sambamba na noti zilizopo kwenye mzunguko,” amemweleza Waziri wa Nchi.

Gavana Tutuba alifafanua kuwa noti hizo zinamwonekano sawa na noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa mwaka 2010, zikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa tu kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.

“Saini ya aliyekuwa Waziri wa Fedha ambaye hivi sasa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Isdor Mpango, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba na saini ya aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania mstaafu, Prof. Florens Luoga, imebadilishwa na kuwekwa saini ya Gavana wa sasa wa Benki Kuu, Bw. Emmanuel Tutuba,” aliongeza.

Akizungumza baada ya kupokea sampuli za noti hizo mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mkuya, amemshukuru Gavana na kumpongeza kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa na kwa kuendelea kuelimisha umma kuhusu masuala mbalimbali ya fedha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news