Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yapeleka Kliniki ya Sheria bila malipo Kilimanjaro, RC Babu aipa kongole

KILIMANJARO-Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mhe.Nurdin Babu ameipongeza na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuuchagua Mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya kutoa huduma ya Kliniki ya Sheria bure kwa wananchi wa mkoa huo.
"Tunaishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma hii bure kwa wananchi wetu hii inaonyesha namna Ofisi hii ilivyojikita kusogeza huduma kwa wananchi kwenye maeneo mbalimbali nchini;

RC Babu ametoa pongezi hizo leo Januari 21,2025 wakati akizindua rasmi Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro katika Ukumbi Mkubwa wa Mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.
Uzinduzi huo, utafuatiwa na Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi inafanyika kwa ushirikiano baina ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya Mkoa wa Kilimanjaro.

Huduma hizi zitatolewa katika Viwanja vya Stendi ya Vumbi jirani na Stendi Kuu ya Mabasi Moshi Mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 21 hadi 27 Januari 2025.

Aidha, Mhe. Mkuu wa mkoa ameeleza kuwa Kliniki hiyo itasaidia kupunguza migogoro ya Wanachi dhidi ya Serikali, zitawezesha Mawakili wa Serikali kusimamia Utawala wa Sheria, pia zitawasaidia Mawakili wa Serikali kushirikiana kwa ukaribu na Wadau pamoja Wananchi katika kutatua masuala ya Kisheria.

"Leo tunakwenda kuanza Kliniki ya Sheria ni matumaini yangu itawasaidia wananchi wenye matatizo ya kisheria, kuna timu nzuri kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali itakuwa inatatua changamoto mbalimbali za wananchi,"amesema Mhe.Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro ametoa wito kwa Wananchi wa Mkoa huo kushiriki kwa wingi katika Kliniki hiyo ili wapate suluhu ya changamoto mbalimbali za kisheria zinazowakabili

Awali akizungumza wakati wa kumkaribisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bi. Tamari Mndeme amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imejipanga vyema kutoa huduma za Kisheria bure kwa wananchi kupitia Kliniki hiyo.
"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iko tayari kuwahudumia Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro na tuna wataalamu wa kutosha tunaamini kupitia Kliniki hii changamoto mbalimbali za wananchi zitatatuliwa," amesema Bi.Tamari.

Kliniki ya Sheria bila malipo kwa Wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro ni mwendelezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika kusogeza huduma za Kisheria kwa Wananchi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news