Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali yazidisha tabasamu kwa wananchi Kilimanjaro, wamiminika Kliniki ya Sheria bure

KILIMANJARO-Wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro wamejitokeza kwa wingi na kufurahishwa na huduma zinazotolewa katika
kliniki ya ushauri wa kisheria bila malipo inayofanywa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa ushirikiano na Kamati ya ushauri wa kisheria ya mkoa wa Kilimanjaro, kliniki hiyo ilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Mhe. Nurdin Babu tarehe 21 Januari, 2025 ambayo itafikia ukomo wake tarehe 27 Januari 2025 katika Viwanja vya stendi ya vumbi Jirani na stendi kuu ya mabasi Moshi.
Wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Bw. Joseph Shoo amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza katika kliniki hiyo ni mzuri, ambapo ameeleza kuwa masuala ya ardhi, mirathi,jinai, ndoa na masuala ya kijinsia ndiyo maeneo ambayo wananchi wengi waliojitokeza wamekuwa wakiyalalamikia na kutaka ushauri wa kisheria.
“Mwitikio wa wananchi ni mzuri tumeweza kupokea malalamiko mengi yanayohusu masuala ya ardhi, mirathi,jinai, ndoa na masuala ya kijinsia. Baadhi ya malalamiko tuliyo yasikiliza tumeyatatua hapahapa na mengine tumeyachukua kwa hatua zaidi. Aidha niendelee kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro wajitokeze zaidi ili tuweze kuwahudumia,”amesema Wakili Shoo.

Akizungumza mara baada ya kupata huduma kwenye Kliniki ya sheria bila malipo, Bw. Mohamed Marandu ameridhishwa na huduma pamoja na maelezo aliyoyapata kutoka kwa Mawakili wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, huku akiamini Kliniki hiyo itawasaidia wananchi wengi kupata haki zao.
“Kupitia kliniki hii nimeweza kupata maelezo mazuri kuhusiana na suala langu la ardhi, Mawakili wamenipokea vizuri na kunieleza hatua sahihi za kufanya ili niweze kupata haki yangu, nawashukuru sana kwa kuja na kutoa elimu hii,”amesema Bw. Marandu.

Kwa upande wake Bi. Emiliana Maliwa ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendesha kliniki ya kisheria bila malipo kwa wananchi kwani Ofisi hiyo imezingatia watu ambao hawana uwezo wa kuwalipa wanasheria katika kuwasimamia masuala yao ya kisheria ya aina zote ili waweze kunufaika na huduma hiyo.
"Niwapongeze na kuishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuleta kliniki hii ambayo inatolewa bure itatusaidia kwakua inatolewa bila malipo yoyote na naamini wengi tutanufaika sana na huduma hii,”amesema Bi. Emiliana.

Katika hatua nyingine akizungumza kuhusu Kliniki hiyo Bw. Isack Ngupa ameiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya kliniki hiyo mara kwa mara na kupeleka huduma hizo za ushauri wa kisheria katika maeneo ya Vijijini ambako wananchi wengi hawana uelewa wa masuala ya kisheria hivyo kupelekea kupoteza haki zao.

“Niwaombe Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuzunguka vijijini kutoa elimu hii, huko kuna changamoto nyingi za kisheria wananchi hawana uelewa wa namna ya kuzitatua, pia watoe huduma hizi mara kwa mara kwani itasaidia sana kupunguza migogoro inayojitokeza katika jamii zetu,”amesema Bw. Ngupa.
Kliniki ya sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Kilimanjaro ilianza tarehe 21 Januari, 2025 inaendelea hadi tarehe 27 Januari, 2025 katika viwanja vya stendi ya vumbi Jirani na stendi kuu ya mabasi ya Moshi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news