ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameeleza kuwa, kuna ongezeko kubwa la wawekezaji katika Sekta ya Utalii hatua inayochangia ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya nchi.
Amebainisha kuwa,ongezeko hilo la wawekezaji pia linachangia ongezeko la watalii wanaotembelea nchini, hali inayoiimarisha Sekta ya Utalii.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo alipoweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hoteli ya SSPD-BUHAIRAN iliyopo Bwejuu Mkoa Kusini Unguja inayomilikiwa na wawekezaji kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu.
Aidha,Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa, faida za utalii ni kubwa kwa nchi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kuwahimiza wananchi kuendelea kuwaunga mkono wawekezaji wanaowekeza maeneo mbalimbali.
Amezitaja faida hizo kuwa ni pamoja na fursa za Ajira kwa Vijana zile za moja kwa moja na nyingine zisizo za moja kwa moja.
Pia,upatikanaji wa soķo kwa bidhaa zinazozalishwa na wakulima na wavuvi kwa bidhaa za baharini na ongezeko la Pato la Taifa.
Halikadhalika Rais Dkt.Mwinyi amewapongeza wananchi wa Bwejuu na Mkoa wa Kusini kwa kuonesha utayari wao na kuwakaribisha wawekezaji hao.
Wakati huohuo Rais Dkt.Mwinyi ameridhia ombi lililowasilishwa na Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja,Ayoub Muhammed Mahmoud kwa niaba ya wananchi la kutengenezewa barabara ya kilomita tatu kwa kiwango cha lami kutoka Michamvi Mashariki hadi Michamvi Magharibi.