CAPE TOWN-Raia wa Japan,Yuji 'Gump' Suzuki mwenye umri wa miaka 34 amewasili mjini Cape Town nchini Afrika Kusini na kuhitimisha safari yake ya kilomita zaidi ya 6,400 kwa miguu kutoka Kenya hadi Afrika Kusini huku akisukuma mkokoteni wake.
Safari hiyo inafikisha zaidi ya kilomita 11,500 alizotembea kwa miguu, baada ya awali kutembea kwa miguu kutoka China hadi India huku akiyazunguka mataifa kadhaa ya Ulaya na kutembea kilomita takribani 5,100 kote nchini Marekani.
Alipowasili eneo la V&A Waterfront mjini humo alipata mapokezi makubwa kutoka kwa raia wa Afrika Kusini ambao walikuwa wakipeperusha bendera za taifa hilo na Japan.
Suzuki mwenye kilo 100 alionekana mwenye hisia kali alipowashukuru wafuasi wake kwa kumuunga mkono katika safari hiyo iliyoanzia katika mji mkuu wa Kenya Nairobi mwezi Julai, mwaka jana ambayo ni zaidi ya siku 210.
"Sijawahi kufikiria kama jukwaa kama hili linaweza kuwepo, kwa hiyo hatua hii ni njema, shukrani kwenu. Asanteni sana kutoka katika moyo wangu wote. Sikuweza kamwe kufikiria kwamba ningesafiri kwa miezi saba."
Aidha, safari yake ilionekana kuwa ya misukosuko, kwani alikumbana na changamoto nyingi za kukosa umeme, kushindwa kuchaji kifaa chochote cha umeme, na kugongwa na lori mara mbili huko Zambia.
Pia, Suzuki alisema kuwa sehemu ngumu zaidi ya safari hiyo ilikuwa ni kupita katika Jangwa la Namibia, kutokana na maeneo mengi ya ardhi ambayo yalikuwa matupu.(NA)