Rais Dkt.Mwinyi aweka jiwe la msingi Barabara ya Kizimbani hadi Kiboje, atoa rai kwa wananchi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewaasa wananchi wa Kiboje na maeneo jirani kuacha kujenga karibu na barabara ili kuepusha athari zinazoweza kujitokeza.
Wito huo ameutoa Kiboje Mamboleo leo wakati akiweka Jiwe la Msingi katika Barabara ya Kizimbani hadi Kiboje yenye urefu wa kilomita 7.225 ikiwa ni sehemu ya kutimiza miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

"Wale ambao wanajenga karibu na barabara tuache kujenga maeneo haya ili tupunguze fidia kwa wananchi na wakati mwingine fidia inakua kubwa kuliko eneo lenyewe," amesisitiza Rais Mwinyi.
Aidha, ameipongeza Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi pamoja na watendaji wake ikiwemo Kampuni ya CCECC kwa kazi kubwa kwa wanayoifanya.

Akitoa taarifa za kitaalamu kuhusu ujenzi wa barabara hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,Dkt.Habiba Hassan amesema, ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025 ya utekelezaji wa taifa wa maendeleo ya usafiri.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayuob Muhammed Mahamud amesema kuwa, maendeleo hayana ushabiki wala dini kwani mkoa wake una miradi 17 ikiwemo ya binafsi miwili, hoteli ambapo moja kuwekwa Jiwe la Msingi na moja imeshafunguliwa na iliyobaki ya umma 

Aidha,amefahamisha kuwa kwa upande wa Sekta ya Umma ni Kituo cha Afya,Mahakama, Kituo cha Magazeti na Kituo cha Kurekebisha Tabia.

Hata hivyo, amesema kuwa kutokana na maendeleo hayo mkoa utaendelea kuyatunza, kuyaenzi na kuyadumisha Mapinduzi ya Zanzibar.
Nao wananchi wa maeneo hayo wamesema kuwa, wamefurahishwa kujengewa barabara hiyo, kwani wataepukana na adha kubwa waliyokuwa wakiipata.

"Sisi wafanyabiashara wa sokoni tulikua waathirika wakubwa kabla ya kujengewa barabara, kwani tulikua tunapata hasara ya kuoza baadhi ya bidhaa zetu ikiwemo ndizi mbivu kutokana na kukosa usafiri," wamefahamisha wakazi hao.
Ujenzi wa barabara hiyo hadi sasa umefikia asilimia 85 ya utekelezaji wake na itagharimu zaidi ya Dola za Kimarekani milioni 6.2 ambapo ujenzi wake umeanza tarehe 17, Novemba 2024 na unatarajiwa kukamilika mwezi Mei 2025.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news