Rais Dkt.Mwinyi aweka jiwe la msingi mradi wa nyumba 370 za makazi Mangapwani, awapa neno wananchi

ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi amewahakikishia wananchi kuwa, Serikali itamlipa kila mwananchi haki yake na hakuna atakayesononeka kwa kukosa fidia.
Rais Dkt.Mwinyi ametoa agizo la kila mwananchi kulipwa kile anachotaka ikiwa ni malipo ya fedha au nyumba.

"Kila mwananchi atalipwa kwa kile anachotaka wa fedha alipwe fedha na anayetaka nyumba atalipwa nyumba,"amesisitiza Dkt.Mwinyi.
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo alipoweka Jiwe la Msingi Mradi wa Nyumba 370 za Makazi ziliopo Mangapwani Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja ikiwa ni nyumba za fidia kwa wananchi walioathirika na ujenzi wa barabara katika Eneo la Mangapwani ikiwa ni sehemu ya ujenzi wa Bandari Jumuishi ya Mangapwani.

Rais Dkt.Mwinyi amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuchangamkia fursa za kiuchumi zitakazokuwepo kwenye miradi mikubwa ya maendeleo iliyopo mkoani humo.

Akizungungumzia ujenzi wa Bandari ya Mangapwani ameeleza kuwa, tayari Mkandarasi amelipwa malipo ya awali na ameanza kazi za upimaji wa sampuli za udongo katika eneo hilo kuelekea kuanza ujenzi.

Vilevile Rais Dkt.Mwinyi ameeleza kuwa, Serikali inakusudia kujenga Uwanja Mkubwa wa Michezo ( Football Academy) katika Mkoa wa Kaskazini Unguja utakaokuwa na viwango vya kisasa.
Rais Dkt.Mwinyi ametoa pongezi kwa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi,Wakala wa Majengo (ZBA) kwa usimamizi mzuri uliofanikisha ujenzi wa nyumba hizo pamoja na Mkandarasi wa ujenzi huo Kampuni ya ORKUN ya Uturuki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news