ZANZIBAR-Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema, ujenzi wa jengo jipya la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) unalenga kuiimarisha mifumo ya ķidemokrasia nchini.
Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo alipoweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Jengo la Afisi Kuu ya Tume ya Uchaguzi huko Maisara Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi.
Rais Mwinyi ameeleza kuwa,kukamilika kwa jengo hilo kutamaliza tatizo sugu la muda mrefu lililoikabili Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) la kutokuwa na eneo bora la kufanyia kazi zake.
Rais Dkt.Mwinyi amefahamisha kuwa, uamuzi wa kulifanya jengo hilo kuwa Kituo Kimoja cha Shughuli zote za Uchaguzi (One Stop Centre) kutaongeza ufanisi kwa watendaji wa tume.
Halikadhalika, Rais Dkt.Mwinyi ameipongeza Tume ya Uchaguzi na Wakala wa Majengo (ZBA) kwa kazi nzuri ya kusimamia ujenzi huo kwa viwango bora na kuhimiza Kampuni ya CRJE ambao ndio wakandarasi wa ujenzi huo kumaliza kazi kwa wakati.
Naye, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa ZEC,Thabit Idarous Faina ameeleza kuwa, ujenzi huo utakamilika na kuanza kutumika kabla ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba,mwaka huu.
Ujenzi wa majengo mawili yenye ghorofa nne utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 11.32 utakapokamilika ambapo ni fedha zilizotolewa na Mfuko Mkuu wa Serikali, kwa sasa ujenzi umekamilika kwa asilimia 81.